Random Posts

VIJIJI 7873 KUPATA UMEME UTEKELEZAJI WA AWAMU YA TATU.

Na Daudi Manongi-MAELEZO
........................
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA),imeanza utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu wa kusambaza nishati vijijini utakaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia mwaka huu wa fedha 2016/17 hadi 2020/21.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-Hanga katika Taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam.

Aidha Taarifa hiyo inasema kuwa vijiji 7697 vitapelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi.

Utekelezaji wa Mradi huu unajumuisha vipengele-mradi  vitatu ambavyo vimelenga kuongeza wigo wa miundombinu ya usambazaji umeme katika maeneo yenye miundombinu ili kufikisha umeme kwenye vitongoji ambavyo havijafikiwa na umeme.Kipengele kingine ni kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme wa gridi na Kipengele cha tatu kinahusisha uzalishaji na usambaji wa nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya umeme wa grid na kwenye visiwa.
Aidha Taarifa hiyo inaeleza kuwa mradi huu umeanza na upo katika hatua mbalimbali ambapo kufuatia Mikataba iliyosainiwa Mwezi Desemba 2016 katika mikoa sita ya Arusha, Iringa, Mara, Mbeya, Pwani, na Tanga kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 27 kutoka Serikali ya Tanzania na Norway, hivyo kuwezesha vijiji 305 kusambaziwa umeme.

Pia umeme utasambazwa kwenye vijiji 3,559 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara unaokadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 733.98 kutoka Serikali ya Tanzania, Norway, Sweden na Benki ya Dunia na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2017/18.
Taratibu za ununuzi zinaendelea na wakandarasi wataanza kazi mwezi Aprili 2017 ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 4,395 kati ya vijiji 12,268 ambayo ni sawa asilimia 36 vimeunganishwa na huduma ya umeme. Baada ya kukamilika kwa mradi huu, jumla ya vijiji 7,934 sawa na asilimia 65 vitakuwa vimefikiwa na umeme. Vijiji 4,334 vinavyosalia vitapelekewa umeme kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2020/21 kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
Kusambaza umeme kwenye vijiji 121 katika maeneo yanayopitiwa na umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 kutoka katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga kwa gharama ya dola za Marekani milioni 30 kwa ufadhili wa Serikali za Norway na Sweden. Taratibu za ununuzi wa wakandarasi zinakamilishwa na utekelezaji utaanza mwezi Machi 2017.
Pamoja na hayo miradi ya umeme wa nje ya Gridi inayotekelezwa na sekta binafsi  imetengewa Jumla ya Dola za Marekani milioni 84 kwa ajili ya mradi huu ambapo kati ya hizo Dola za Marekani milioni 42 ni kutoka Serikali ya Uingereza na Dola za Marekani milioni 42 kutoka Benki ya Dunia.  Wakala ulitangaza awamu ya kwanza ya mradi huu tarehe 23 Septemba, 2016 kwa ajili ya kushindanisha waendelezaji binafsi na wajasiriamali wa nishati jadidifu kwenye maeneo ya nje ya gridi na Awamu ya pili itatangazwa mwezi Aprili 2017, matangazo haya yatakuwa yanatolewa kwa awamu kila baada miezi sita. Wajasirimali wa nishati jadidifu wanahamasishwa kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu. 

Wakala unaishukuru Serikali kwa kuweka msisitizo kwenye miradi ya usambazaji wa nishati bora vijijini pamoja na kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara ifikapo Mwaka 2021; na kuongeza idadi ya vijiji vilivyofikiwa na huduma ya umeme hadi asilimia 85 mwaka 2025 na asilimia 100 Mwaka 2030.

Post a Comment

0 Comments