Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Pof.Elisante Ole Gabriel akizungumza na Wasanii (hawapo pichani )
katika uzinduzi wa programu ya kuuza muziki na filamu kupitia mtandao
(online)iliyoandaliwa na Kampuni ya Afroprimiere jana Jijini Dar es
Salaam.Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi maendeleo ya Sanaa Hajjat Shani Kitogo na wa kwanza Kulia ni
Bw.Fredy Ngimba Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo.
Baadhi ya Wasanii walioshiriki katika uzinduzi
wa programu ya kuuza muziki na filamu kupitia mtandao (online) iliyoandaliwa na
Kampuni ya Afroprimiere jana Jijini Dar es Salaam.
.......................................................................................
Na Shamimu Nyaki.
Serikali kupitia
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa agizo kwa wasanii wa hapa
nchini kutumia lugha fasaha ya Kiswahili katika kazi zao ili kuitangaza lugha hiyo
inayotambulisha Taifa letu.
Agizo hilo limetolewa
jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizindua program ya kuuza muziki
na filamu kwa njia ya mtandao iliyoandaliwa na Kampuni ya Afroprimiere.
Prof. Gabriel alisema
kuwa Tanzania inatambulika Duniani kwa lugha ya Kiswahili hivyo wasanii wana
nafasi kubwa ya kuendelea kutumia lugha hiyo kwa ufasaha katika kazi zao
wanazofanya ili kukuza lugha ya Kiswahili.
“Wasanii mnafanya
kazi zenu kwa Kiswahili ni vyema mkatumia lugha hii kwa ufasaha zaidi lakini
pia kuweni sehemu ya mafanikio ya mpango huu ili mfanikiwe zaidi.” Alisema
Prof. Elisante.
Aidha amewahakikishia
wasanii kuwa Serikali itaendelea kutunza haki za wasanii na kuwaunga mkono
katika programu hii ili iwe na faida kwa Serikali katika kupata mapato na
wasanii pia kupata faida ya kazi zao.
“Kutunza Kazi za
wasanii ni jukumu letu, nawahakikishia hakuna atakayekosa faida katika jambo
hili kama tutakua pamoja na kushirikiana.” Aliongeza Prof Gabriel.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Afroprimiere ambao ndio waandaaji wa program
hiyo Bw. Fredy Ngimba amesema kuwa program yao inalenga kuwasaidia wasanii
namna wanavyoweza kufaidika na biashara
ya kazi zao mtandaoni.
“Programu hii
itawasaidia wasanii kujua idadi kamili ya wanunuzi wa kazi zao mtandaoni na
namna ambavyo watagawanya mapato kwa wote wanaohusika kuanzia Serikali, Waandaji,
Watengenezaji na wasambazaji wa kazi hizo.”Alisema Bw. Ngimba.
Mapato kwa wote
wanaohusika katika kazi hiyo yanaonyesha kuwa Msanii ambaye ndio mwenye kazi
yake atapata 50%, Muandaaji 25%, Kampuni ya Mawasiliano 20%, mtengenezaji 08%
na Serikali 18%.


0 Comments