Na Frank
Geofray-Jeshi la Polisi.
Maofisa wakuu wa
Polisi wanatarajia kukutana mkoani
Dodoma kuanzia jumatatu tarehe 27-29/03/2017 katika kikao kazi cha siku tatu
kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu na wahalifu
hapa nchini.
Akizungumza na
Waandishi wa habari ofisini kwake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Advera
Bulimba alisema kikao hicho kitawakutanisha maofisa wakuu wa makao mkauu ya
Polisi, makamanda wa Polisi wa mikoa na Makamanda wa vikosi bara na Zanzibar
ili kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utendaji katika
kipindi cha mwaka uliopita na kuweka mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa
mwaka 2017.
Aidha, Bulimba
alisema mbali na utaratibu wa mawasiliano ya kila siku katika kuimarisha
usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi pia lina utaratibu wa kukutana
kila mwaka kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu kukabiliana na wahalifu kwa
lengo la kuhakikisha kuwa usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika hapa
nchini.
“Katika kikao
hicho Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu atatoa maelekezo ya
kiutendaji ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa kila ofisa, mkaguzi na askari anawajibika kwa nafasi yake
katika kuhakikisha uhalifu unapungua hapa nchini” Alisema Bulimba.
Bulimba alisema
kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhe.Mwigulu Nchemba ambapo kauli mbiu katika kikao hicho ni “Zingatia maadili
tunapopambana na uhalifu ili kuimarisha usalama kwa maendeleo ya Taifa”.
0 Comments