Na: Lilian Lundo –
MAELEZO.
........................
Ofisi ya Makamu wa
Rais Mazingira ikishirikiana na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
leo imefanya operesheni kwa baadhi ya wasambazaji wa pombe za kali
zinazofungashwa katika plasti maarufu kama kiviroba ili kujiridhisha kama
wameitikia wito wa kusitisha utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa pombe hizo.
Akiongea na vyombo
vya habari Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard
Muyungi amesema kuwa operesheni hiyo imeanza na wasambazaji, wauzaji na
watumiaji huku wakiendelea kupitia baadhi ya maombi ya wamiliki wa viwanda juu
ya usitishaji wa pombe hizo.
Aidha operesheni hiyo
imefanyika katika wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala kwa kutembelea maghala
yanayohifadhi pombe hizo ili kujua idadi ya pombe ambazo bado zipo katika maghala
hayo pamoja na kufuatilia ikiwa wamiliki wa maghala hayo wametii amri ya kusimamisha
usambazaji wa Pombe hizo zilizofungiwa kuanzia Marchi 01, 2017.
Msimamizi wa ghala la
Pombe za Viroba aina ya Kiroba Original
lililopo Mabibo wilaya ya Kinondoni Mhina Rashid amesema kuwa akiba ya pombe hizo
za viroba zilizobaki katika maghala yao ni katoni 6600 za ujazo wa Ml 50 na katoni 4909 zenye ujazo
wa Ml100.
“Kwa sasa tumefunga maghala
na hakuna usambazaji wowote wa pombe aina ya kiroba unaofanyika hapa tunasubiri
taratibu za Serikali kujua nini cha kufanya kwa pombe ambazo bado zipo katika
maghala,” alifafanua Mhina Rashid.
Aliendelea kwa kusema
kuwa ikiwezekana Serikali iongeze muda wa matumizi ya pombe hizo kutokana na
kuwa na mzigo mkubwa katika maghala mengi yanayohifadhi pombe hizo.
Kwa upande wake,
Afisa Mwandamizi wa Viwango na Mkaguzi wa TBS Banza Suleiman amesema kuwa
viroba Original vina nembo ya TBS lakini kutokana na sheria mpya ambayo imepiga
marufuku matumizi ya pombe hizo hivyo wasambazaji hawaruhusiwi kusambaza pombe
hizo bali wanapaswa kusubiri maelekezo toka Serikalini.
Vile vile operesheni
hiyo imefanyika katika kiwanda cha Afro American kilichopo Mwenge ambao ni
watengenezaji wa pombe za viroba aina ya Zed, Royal na Dollors na kukuta zaidi
ya tani 5 ya pombe hizo.
Msimamizi wa kiwanda
hicho Muhandisi Sabra Voleti amesema kuwa wamesimamisha uzalishaji wa pombe za
viroba huku wakisubiri maelekezo toka Serikalini. Aidha amesema kuwa kiwanda
hicho kinaendelea na uzalishaji wa pombe ambazo vifungashio vyake ni vya chupa.
Kwa upande wake Mwanasheria
wa NEMC Manchare Heche Suguta amesema kuwa adhabu ya matumizi ya vifungashio
vya plastiki (Viroba) vinatofautiana kati ya mtengezaji, msambazaji, muuzaji na
mtumiaji. Aidha adhabu yake ni faini kati ya shilingi elfu 50 na Milioni 5 au
kifungo kisichopungua miaka 3.
Hivyo amewataka
watanzania kujiepusha na matumizi ya pombe hizo pamoja ikiwa ni pamoja na
utengenezaji na usambazaji wake.
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani
Manyara Februari, 2017 aliagiza pombe hizo kutoendelea kutumika kuanzia Marchi
1, 2017.
No comments:
Post a Comment