Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, wazee na watoto imebainisha kuwa inatarajia kuwapeleka Madaktari
wake waliopo nchini Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya kufuatia kuombwa
na Rais wa nchi hiyo Mhe. Uhuru Kenyatta.
Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo, Waziri wa Afya,
Mh. Ummy Mwalimu amesema kuwa, ujumbe maalum kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta
kupitia kwa Wiziri wake wa Afya uliokutana na Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli na kuomba ombi lao hilo la
kutaka madaktari 500, ambao wataajiliwa kwa mikataba maalum ya kuanzia miaka 2
kwa kufanya kazi nchini Kenya.
“Natoa rai kwa madaktari wazawa waliopo nchini kuomba nafasi
za ajira ya Udaktari nchini Kenya kwa
mkataba maalum. Zoezi hilo limeanza rasmi leo Machi 18 mpaka Machi 27, mwaka
huu wawe wameomba.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa waombaji ni wale watakaokidhi
vigezo maalum ikiwemo asiwe katika utumishi wa Umma, Asiwe amejiliwa na
mashirika ya umma ama mashirika teule ambayo yanalipiwa na Serikali.
Kwa Mujibu wa Waziri Ummy ameeleza kuwa muombaji lazima awe
amehitimu mafunzo ya “internalship” na mwisho awe amesajiliwa na baraza la
Madaktari nchini.
Aidha, Waziri Ummy ameweka wazi kuwa, ajira hiyo itakuwa ni
ya miaka miwili ambapo watapata mishahara na malupulupu mbalimbali katika ajira
zao hizo huku akibainisha kuwa, jambo hilo ni jema na linaiingizia Taifa sifa
kwa kupeleka wataalamu wake nje ya nchi kupata ajira.
Kwa upande Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mpoki
Ulisubisya amesema kuwa, moja ya vigezo ambavyo vinahitajika kwa madaktari hao
ni pamoja na kuwa na digrii ya kwanza na Internal ship huku akiongeza kuwa, kwa
upande wao Wizara imejipanga kuimalisha madaktari wa ndani ikiwemo kiwaajili.
Naye Katibu Mkuu Utumishi, Mh. Laulian Ndumbalo amewatoa
hofu watanzania licha ya kuwapeleka Madaktari hao nje kupatiwa ajira, nchini
bado ina Madaktari wengi wanaofikia zaidi ya 1000, huku kila mwaka wakiajili
Madaktari 400 hadi 450.
Imeelezwa kuwa Madaktari
hao watakaojitokeza watapata faida kubwa kwani watakuza mahusiano mema ya nchi
za Afrika Mashariki kupitia kada hiyo huku pia wakitarajia kuipatia maendeleo
nchi ya Tanzania. Jambo ili ndio la kwanza linafanyika huku ikielezwa kuwa
idadi hiyo ya madaktari kutoka Tanzania kwenda kupatiwa ajira nje ya mipaka
yake ni kubwa, licha ya madaktari wengi kuwepo nchi mbalimbali ikiwemo Malawi,
Zambia, Afrika Kusini, Botswana na mataifa mengine.
Madaktari hao wenye kutaka kujiunga wanaweza kutembelea
tovuti ya wizara ya Afya na kupata maelezo mbalimbali.

0 Comments