Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Kikao cha Kazi cha
Mawaziri alichokiitisha kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Machi 3,
2017.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
...........................................................
JUMLA
ya watumishi wa umma 2,059 wamekwisharipoti Dodoma katika awamu ya
kwanza ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Magufuli aliyoitoa wakati akikabidhiwa uenyekiti wa CCM, Julai 22,
mwaka jana.
Awamu
ya kwanza ya Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma inajumuisha Mawaziri
na Manaibu wao, Makatibu Wakuu na manaibu wao, baadhi ya wakurugenzi
pamoja na wasaidizi wachache.
Hayo
yamebainika leo (Ijumaa, Machi 3, 2017) katika Kikao cha Kazi cha
Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
Hazina mjini Dodoma chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka Mawaziri wote watoe taarifa za idadi
ya watumishi wao waliohamia Dodoma hadi sasa, wamepanga kufanya zoezi
hilo kwa awamu ngapi na lini watakamilisha zoezi hilo. Pia Mawaziri hao
walitakiwa kueleza mahali zilipo ofisi zao kwani amepanga kuwatembelea
na kuzungumza na watumishi.
Wakiwasilisha
taarifa hizo, Mawaziri hao wote wamethibitisha kwamba tayari ofisi zao
na wao wenyewe wameshahamia Makao Makuu Dodoma pamoja na watumishi wao
wote walioko kwenye awamu ya kwanza na wameahidi kukamilisha kuhamisha
waliosalia katika awamu nne hadi sita kulingana na ratiba ya Serikali.
Aidha,
Waziri Mkuu amesema baada ya Serikali kukamilisha ratiba ya kuhamia
Makao Makuu Dodoma, Jiji la Dar es Salaam litabakia kuwa Jiji la
kibiashara na wamepanga kuendelea kuendelea kuliboresha ili shughuli
hizo zifanyike kwa ufanisi zaidi.
Mapema,
akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua kikao hicho, Waziri
Mkuu alisema kati ya Julai 2016 na Januari 2017, Tume ya Kudhibiti Dawa
za Kulevya iliwakamata watu 11,303 ambao wanatuhumiwa kujihusisha na
uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema
kati ya hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174
wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa
kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka
huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao
unaendelea.
“Wengi
kati ya hao, wameshikwa na vithibitisho, ingawa uchunguzi wa kesi zao
bado unaendelea. Na hawa ni wale waliokamatwa na dawa za viwandani kama heroine na cocaine.
Hatujawaingiza wale waliokamatwa na mirungi au bangi.
Bado mikoa
inaendelea na kazi, na hii operesheni ni ya nchi nzima,” alisema.
Uamuzi
wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi,
1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
Tangu
wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za
kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa
uwekaji wa miundombinu hiyo.
Serikali
ya awamu ya tano iliamua kuhamia Dodoma baada ya kuridhishwa na ujenzi
wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na
wenyeji.


0 Comments