NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi CCM
Zanzibar, kimeendelea kuweka wazi msimamo wake
kuwa hakiwezi kukaa meza moja na CUF kuzungumzia Uchaguzi wa mwaka 2015 na
Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK) bali kipo tayari kukaa na chama hicho
kujadili changamoto zinazowakabili wananchi.
Msimamo huo umetolewa na Naibu Katibu
Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Abdallah Juma Saadalla “Mabodi” katika Mahojiano Maalum kuhusu masuala ya hali ya Kisiasa, Kiuchumi
na Kijamii nchini huko Afisini Kuu CCM Kisiwandui, Unguja.
Alisisitiza kwamba mjadala wa mambo hayo, umefungwa toka Machi 20, mwaka 2015 katika
Uchaguzi wa marudio, hivyo kwa sasa CCM inasimamia serikali zake zitekeleze kwa uhakika na haraka Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 12015/2020, kwa
wananchi wote bila ubaguzi.
Dkt. Mabodi alisema kitendo cha
kuendelea kujadili Uchaguzi uliopita ambao mwanzo
ulifutwa kisheria na kurudiwa tena ni kudhalilisha Katiba
ya nchi, jambo ambalo CCM haipo tayari kwani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.
Ali Mohamed Shein na Watendaji wake wameingia madarakani kwa misingi ya
Kidemokrasia Kanuni na sheria za nchi na Dunia yote inajua hivyo.
Hoja hizo zimekuja baada ya siku za
hivi karibuni pindi ujumbe wa Ubalozi wa Marekani kufanya mazungumzo na Chama
hicho, na baadae baadhi ya Magazeti na Mitandao ya kijamii
kupotosha mazungumzo hayo kwa kudai kuwa upo uwezekano vya vyama hivyo viwili
kurudi katika meza ya mazungumzo kujadili Suala la Uchaguzi uliopita na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia alisema Chama hicho kipo tayari wakati wowote kuzungumza na Chama
chochote cha kisiasa, na nchi mbali mbali Duniani juu ya kujadiliana mikakati
na mbinu endelevu ya kutatua matatizo na kero za wananchi hasa wa baadhi ya
Majimbo ya Pemba yasiyokuwa na maendeleo licha ya kuwa na Wabunge wanaotoka
CUF, waliowasusia wapiga kura wao na mzigo wote kuwaachia Wawakilishi na
madiwani wa CCM pekee.
“ Naomba Wapinzani wetu waelewe kwamba
Zanzibar ina mihimili mitatu ya Dola ambayo ni Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama, vyombo hivi vipo kisheria
vikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein na Baraza lake la Mawaziri, sasa
mnataka tujadili nini tena.
Pia kwa lugha rahisi na inayoeleweka
zaidi ni kwamba Safu hiyo itaendelea kubaki madarakani mpaka 2020, hakuna
miujiza wala taifa lolote Duniani la kuingilia siasa zetu za ndani”.,
alisema Dkt. Mabodi na kuwataka wanasiasa
kuwa wakweli na wenye utu na huruma za kupigania wapiga kura wao wawe na maisha
mazuri, na kuondokana na siasa za jino kwa jino, chuki na migogoro.
Huduma za kijamii
Alisema serikali inayotokana na CCM
kupitia Dkt. Shein imeimarisha huduma za afya sambamba na kuongeza vifaa tiba
vya kisasa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na Pemba Hospitali ya Abdalla
Mzee huku ikiboresha kitengo cha upasuaji wa matatizo ya Uti wa Mgongo, Kichwa
kikubwa, Mishipa ya fahamu na saratani ya
Ubongo matibabu hayo yote yanafanyika Zanzibar Mnazi
Mmoja bure.
Kwa upande wa sekta ya elimu serikali
imeimarisha ngazi za elimu ya Awali hadi Vyuo vikuu ambapo kwa sasa inazalisha
wataalamu wa fani mbali mbali hapa nchi huku wengine wakipata mafunzo yao nje
ya nchi.
Aidha kumeimarishwa Sekta za Uvuvi,
Ufugaji na kilimo cha kisasa ambapo wananchi wanapata huduma za Pembe jeo na
kwa gharama nafuu na bure kwa wakati mwingine , huku wakilimiwa na Matrekta ya
kisasa.
Kwa upande wa miundo mbinu ya
serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa viwanja
vya ndege na bandari za kisasa na kuruhusu wawekezaji katika usafiri wa
baharini na makampuni ya ndege huku imejenga barabara za kiwango cha lami Unguja na
Pemba mjini na vijijini ili wananchi wapate unafuu wa kutoa mazao yao
mashambani hadi sokoni kwa urahisi.
“ Wabunge wote ndani ya Bunge la
jamhuri ya Tanzania wanapokea Mafao, sitahiki, mishahara na fedha za majimbo
sawa , lakini cha kusikitisha wenzetu wanaporudi
majimboni wanadai kuwa serikali ya CCM ndio yenye dhamana ya kutatua kero za wananchi,
sio kwamba tumechoka tunaendelea kufanya na tunafanya mpaka katika makaazi
yao.” Alisema Dkt. Mabodi na kuongeza kuwa wapinzani wanakimbia majukumu yao
kwa kutotekeleza yale waliyowaahidi wapiga kura wao.
Hali ya Kisiasa Zanzibar.
Dkt. Mabodi alisema hali ya kisiasa
Zanzibar kwa ujumla ipo shwari licha ya kuwepo
kwa changamoto za baadhi ya wanasiasa kutokubali mambo mema yanayosimamiwa na
CCM katika utekelezaji wake.
Lakini alieleza kwamba Chama hicho
hakitochoka kuwaelimisha kwani baadhi yao tayari wameanza kuhama ndani ya CUF
na kujiunga na CCM, katika maeneo mbali mbali nchini na hivi karibuni wamepokea
wanachama Wapya zaidi ya 90 huko Jimbo la Makunduchi waliovutiwa na Sera, na
siasa za Chama Cha Mapinduzi, waliodai kuwa wamechoshwa na sera za CUF
zisizotekelezeka.
Alisema kwamba kila nchi
duniani ina mifumo yake ya kiutawala hivyo katika
ulimwengu wa Kidemokrasia lazima uwanja wa siasa uwe na faida na kasoro za hapo
na pale kwani sehemu yoyote yenye pande mbili zinazopingana kimisimamo lazima
hayo yatokee lakini ni mambo yanayozungumzika.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema
SUK iliwekwa na wananchi wa Visiwa vya Zanzibar na wakati ukifika wakaamua
wenyewe kuiondosha au ibaki na kueleza kuwa yeye sio mingoni mwa fikra za
wapinzani wanaoamini kuwa Utulivu na Amani ya Zanzibar vipo kwa ajili ya mfumo huo bali anachokiamini ni kwamba Wananchi wamekuwa waelewa zaidi na kupima katika uzani kuwa ni
siasa zipi wazifuate ndipo walipamua dhana hizo kwa kuzika siasa za Chuki na Marumbano.
“ Kipindi tupo katika SUK Zanzibar
yalitokea matukio mengi ya kutisha Zanzibar ambayo kihistoria hayakuwahi
kutokea na huwa sipendi kuyakumbusha ila nitatoa mifano, kuwa matukio hayo ni
pamoja na kujitokeza vikundi vya Kihalifu kama Mbwa Mwitu, viongozi wa dini
kuuawa na kumwagiwa Tindi kali pamoja, kuchomwa kwa Makanisa, kuchomwa kwa
Matawi na Ofisi za CCM, uhalibifu wa miundombinu na baadhi ya wananchi kuigomea
serikali.” Alifafanua Dkt. Mabodi na kuhoji kuwa
vitendo hivyo wakati vinatokea Wenzetu tulikuwa katika serikali Kitaifa SUK,
hakuna hata kiongozi hata mmoja aliyekemea wala kulaani uhalifu huo.
Siri ya CCM kuwa imara kwa miaka 4O.
Mwanasiasa huyo alisema kufanikiwa kwa Chama hicho kunatokana na
radhi za Wazee wa Chama hasa wale walioasisi vyama vya ASP na TANU, ambao
miongozo waliyoiacha mpaka sasa bado inaimarishwa tena kwa mifumo ya kisasa.
Pia alisema kwamba sababu nyingine ya
kuaminika kwa chama hicho inatokana na muundo wake ambao umejitawanya kuanzia
ngazi za mashina ( Nyumba kumi) hadi Taifa zote hizo zinakuwa na viongozi
wanaochaguliwa Kidemokrasia hali ambayo ni tofauti na vyama vingine
vilivyojenga safu za uongozi kwa ngazi za juu pekee.
Hali ya kiuchumi
Naibu huyo ambaye amewahi kufanya
kazi katika taasisi za kimataifa, alisema kwamba
uchumi wa Zanzibar unakuwa kwa kasi kutokana na usimamizi mzuri wa ukusanyaji
wa mapato, unaotokana na usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi zinazoendana na matakwa ya
sasa ya kuelekea katika falsafa za Zanzibar yenye viwanda.
Aliwashauri wananchi kutumia vizuri
fursa na mazingira bora ya kimiundo mbinu yaliyowekwa na serikali kwa kufanya
kazi kwa bidii hasa zile za uzalishaji mali ili waweze kuchangia ukuaji wa
uchumi wa nchi.
Aliwaomba Wananchi kuunga mkono
juhudi zinazofanywa na Marais wa pande zote mbili ambao ni Rais wa Zanzibar
, Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kasi zao nzuri za kiutendaji juu ya
maendeleo ya nchi.
Aidha alisema Zanzibar imepata neema ya Uchimbaji na utafutaji wa rasilimali za Mafuta
na gesi asilia ambazo kwa sasa tayari zimeanza kwa nchi nzima, hivyo wananchi
watoe ushirikiano kwani fursa hiyo ni moja ya vitega uchumi muhimu vya kitaifa,
lakini wasisahau kujiimarisha katika sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji.
Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF kwa sasa
Naibu Katibu Mkuu
huyo alisema hawezi kuzungumzia sana mgogoro huo kwani haubebi dhamira ya
kutatua kero za Wanzania, bali unaendelea kukuwa kutokana na baadhi ya viongozi
wa Chama hicho kugubikwa na uchu wa madaraka na Utawala huku wakisahau kwamba
fursa hizo zinatokana na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.
Aidha alisema huu ndio
wakati mwafaka wa Watanzania kupima siasa za Vyama vya Upinzani na badala yake
wakafanya maamuzi sahihi ya kuviacha na kujiunga na CCM chama ambacho kauli na
vitendo vyake vinahimiza Amani, Mshikamano na Umoja sambamba na kueneza sera za
maendeleo kwa wananchi wote.

0 Comments