Uongozi wa wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani wakisikiliza kero mbalimbali za migogoro ya ardhi kutoka kwa wananchi huko makazi mapya, kitongoji cha Kimara, Msongola Kibaha Vijijini.
Mzee Hendric Simba ,mkazi wa Ngeta akitoa kilio chake kutokana na mgogoro wa ardhi ambapo ulisababisha uongozi wa wilaya ya Kibaha kwenda huko Makazi Mapya, Msongola Kibaha Vijijini kusikiliza kero mbalimbali za migogoro ya ardhi.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
........
Na
Mwamvua Mwinyi,Kibaha Vijijini
SERIKALI ya wilaya ya
Kibaha, imerejesha hekari 89 mikononi mwa serikali ya kitongoji cha Makazi
Mapya Msongola ,kata ya Kawawa,Kibaha Vijijini kwa ajili ya huduma za kijamii
ikiwemo kujenga shule, zahanati.
Ardhi hiyo imerejeshwa
kwa wananchi baada ya kukaa kipindi kirefu pasipo kuendelezwa.
Aidha serikali hiyo
imewataka wakazi wa makazi mapya Msongola kuacha kukumbatia ardhi kuanzia
hekari moja hadi 50 -100 pasipo kuziendeleza .
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka serikali ya wilaya, ilisema hadi ifikapo June mosi mwaka huu,
asiyeendeleza atapokonywa ardhi hiyo.
Nae afisa tarafa ya
Kibaha Anatory Mhango akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ngeta ,Kimara na
makazi mapya,alikemea tabia ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuuza maeneo
kinyume na taratibu kwa kujinufaisha wenyewe.
Afisa tarafa huyo,
ambae alikuwa akikaimu nafasi ya katibu tawala wilaya ya Kibaha, alieleza,
uongozi wa vijiji hivyo usioze ardhi ya vijiji kuanzia sasa.
Mhango alisema uuzaji
huo holela unaofanywa na wenyeviti hao umekuwa ukisababisha migogoro baina ya
mtu na mtu ama mtu na mwekezaji kutokana na kuuziwa eneo moja.
Alisema tabia hiyo
imekuwa ikiwapa kero wananchi ambao wamekuwa wakiuziwa eneo moja wawili au
kuuziwa mara mbili.
Katika hatua nyingine
serikali ya wilaya hiyo, imekata mzizi wa fitina kwa kumaliza migogoro ya
baadhi ya wakazi waliokuwa wakigombania ardhi,ikiwemo eneo la Hendric Simba.
Moja ya mgogoro
uliokuwepo ni wa wakazi wanaoishi kijiji cha Ngeta ambao walikuwa wakililia
warudishiwe ardhi yao ya asili iliyopo kitongoji cha Kimara , ilichukuliwa
mwaka 1974 katika operesheni vijiji.
Wakazi hao wametakiwa
kuridhika na ardhi waliomegewa eneo la kitongoji cha Kimara .
Hata hivyo
wamerejeshewa eneo la makaburi yao ya asili ambapo watatakiwa wazungushie uzio
ili lisiingiliane na maeneo waliyogawiwa watu wengine.
Awali mwenyekiti wa
wakazi wa asili,Hendric Simba alisema wakati wa operesheni vijiji walihamishiwa
katika kijiji cha Ngeta ambapo hawakuridhishwa kutokana na kupewa maeneo madogo
yasiyolingana na waliyokuwa nayo awali.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Makazi Mapya,Omari Kipuga alisema kitongoji cha Kimara kimeanzishwa mwaka 2006 kutoka kitongoji cha Makazi Mapya ambacho kipo kihalali.
Alisema operesheni
vijiji ilifanywa kisheria na wakazi hao walihamishwa na kupelekwa maeneo ya
Ngeta,Dusinyara,kikongo na Mwanabwito.
Kipuga alibainisha,
eneo la Makazi Mapya limezalisha kitongoji cha Kimara,kata ya Kawawa,limepimwa
kisheria na maafisa wa halmashauri ya Kibaha lina hekta zaidi ya 2,000 na
wakazi wanaoishi kisheria 1,500.



0 Comments