MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo.
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani,
mhandisi Evarist Ndikilo, ameweka wazi kuwa, oparesheni inayoendelea kufanyika
wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga hazipo kwa ajili ya kumnyanyasa mtu.
Amesema wananchi waache
polisi na serikali ifanye kazi na doria ili waweze kuwapata wahalifu
waliohusika katika matukio ya mauaji yaliyowahi kutokea.
Mhandisi Ndikilo alieleza,
kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuwa wananyanyaswa na polisi
hao.
Alibainisha kwamba, jamii
ijenge ushirikiano na jeshi la polisi pamoja na serikali kwa kuendelea kuwataja
wanaowadhania ni wahalifu au wauaji badala ya kuwanyooshea kidole askari
polisi.
Mhandisi Ndikilo, alisema
matukio hayo ni ya kipindi kirefu yanayohusisha kuuwawa wenyeviti wa vijiji,
vitongoji na askari polisi hivyo ni wakati wa kuachia vyombo vya dola vifanye
kazi yake.
"Kuna malalamiko
nimefikishiwa kutoka kwa baadhi ya watu wakidai wananyanyaswa na polisi,
hapana, niwaombe wananchi waliopo Kibiti na Rufiji ukiambiwa na polisi simama
basi usimame, ukihojiwa basi jibu kuliko kukimbia "
"Ukikimbia nyumba
yako ,mji wako, unaweka alama ya kuuliza kuwa taarifa inazozipata polisi
kupitia jamii yenyewe basi ni kweli, kama wewe sio mhalifu kwa nini ukimbie
"alisisitiza .
Mkuu huyo wa mkoa ambae
pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa, alielezea kwamba,
oparesheni inayoendelea haitamwonea mtu yoyote kwani inafanywa kwa kuzingatia
sheria.
Mhandisi Ndikilo alisema
ulinzi umeimarishwa zaidi na aliomba kama kunatokea tetesi ama malalalamiko
yoyote lijulishwe jeshi la polisi na serikali ya mkoa ili itoe ufafanuzi wa
kina.
Nae kamanda wa polisi
mkoani Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi, Onesmo Lyanga, alisema polisi
linafanya kazi yake kwa kulinda amani,wananchi na mali zao.
Alisema watapambana
usiku na mchana hadi watakapohakikisha mtandao wa wahalifu unakamatwa .
Lyanga alisema kuwa
wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili viweze kufanya
kazi zake vizuri.

0 Comments