Timu ya soka ya taifa ya vijana
chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imedhihirisha ubabe wake kwa
wenyeji wa fainali za U-17 Afrika mwaka huu, Gabon baada ya kuwafunga
tena 2-1 katika mchezo wa kirafiki mjini Rabat.
Mabao ya Serengeti Boys yamefungwa na Assad Juma na Abdul
Hussein na hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo vijana wa Tanzania
wanawapa wavulana w Gabon, baada ya Aprili 22 kuwafunga pia 2-1, mabao
ya Kelvin Nashon Naftali dakika ya 18 na Ibrahim Abdallah Ally dakika ya
75.
Serengeti Boys imeweka kambi ya
mwezi mmoja nchini Morocco kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zinazotarajiwa kuanza Mei
14 hadi 28, mwaka huu nchini Gabon.
Kwa ujumla huo unakuwa mchezo wa tano wa maandalizi kwa
Serengeti kujiandaa fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi
mara mbili, Machi 30 mabao 3-0 na Aprili 1 mabao 2-0, mechi zote mbili
zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2
na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serengeti Boys itakuwa kambini mjini Rabat hadi Mei 1, mwaka
huu itakapowenda Younde, Cameroon kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi
ya wenyeji Mei 3 na 6, mwaka huu.
Mei 7 timu hiyo itakwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja
na timu za Mali, Niger na Angola, wakati Kundi A lina timu za wenyeji,
Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.

0 Comments