Rais Mstaafu wa Awamu
ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Benjamin William Mkapa amewataka viongozi wa nchi kuzingatia maadili
na miiko ya uongozi ikiwa ni njia ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius
Kambarage Nyerere.
Rai hiyo imetolewa
leo wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Mwl Nyerere
lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mkapa alisema kuwa katika
kumuenzi Mwl. Nyerere ni vyema viongozi
wakamuenzi kwa kufuata maadili na miiko ya uongozi jambo litakalo pelekea kuwa
viongozi bora katika jamii.
“Urithi wa Mwl.
Nyerere katika uongozi ni kufuata yale aliyokuwa akiyafanya na katika uongozi
wake aliweza kutekeleza na kuzingatia maadili na miiko ya uongozi kwa kuwaongoza
wananchi kwa usawa na haki, hivyo katika
kumuenzi hatuna budi kufuata yale aliyoyafanya, ” alisema Mkapa.
Aidha Mkapa alitoa
pongezi kwa uongozi wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuweza kukiinua tena
chuo hicho kwani kipindi cha kati chuo kililega na kupoteza mwelekeo.
Pia aliwataka Watanzania
kuacha kubuni mambo wasiyoyajua na badala yake wapende sana kusoma na kuelewa
historia ya nchi na Serikali kwa ujumla
ikiwa ni njia mojawapo ya kumuenzi baba wa Taifa.
“Napenda kuwasihi Watanzania
wapende sana kusoma ili kuweza kutanua upeo wao wa kufikiri kwani Baba wa Taifa
alipenda sana kusoma makala za ndani ya nchi, vitabu na makala za nje ya nchi
ili kuweza kupanua upeo wake kwa ajili ya kutatua matatizo ya hapa na matatizo
ya Kimataifa” aliongeza Mkapa.
Kwa upande wake Waziri
Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba alisema kuwa sifa za uongozi bora ni
pamoja kuthamini utu, uzalendo, uchapakazi na aliye na hofu ya Mungu.
“Sifa ya kiongozi
bora ni lazima awe mtu anayethamini utu wa mtu na anayeamini binadamu wote ni
sawa, awe mzalendo, muadilifu, mchapa kazi na ana hofu ya mungu,anashirikiana
na kuwashirikisha viongozi wenzake." Alisema Jaji Warioba.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Phillip
Mangula alisema kuwa cheo ni dhamana unayopewa na wananchi hivyo kiongozi bora
ni yule atakaye ongoza kwa usawa.
”Cheo ni dhamana
unayopewa na wananchi ili uweze kuongoza kwa usawa kwani kiongozi bora
atawaongoza watu kwa usawa,” alisema Mangula.
Mangula alisema kuwa
katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi anayejali
sana wananchi wake akiamini kuwa binadamu wote ni sawa jambo ambalo analiona linajirudia
katika Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye
naye amejipambanua kwa kuwajali wanyonge.
Kongamano hili
lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu wakiongozwa na Rais Mstaafu
Benjamin Mkapa, Salim Ahmed Salim,Spika Mstaafu Anne Makinda, Jaji Warioba,
Jaji Agustino Ramadhan, na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini.Kauli
mbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Urithi
wa Mwalimu Nyerere Katika Uongozi, Maadili ya Uwajibikaji Kwenye Ujenzi wa
Taifa.”


0 Comments