Na
Shanni Amanzi
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)Selemani Jafo amemtaka
Mkurugenzi wa Wilaya ya Chamwino Athuman Masasi kuhakikisha kuwa Mradi wa maji
wa kijiji cha Manzase unamalizika ifikapo mwishoni mwa mwezi mei, mwaka huu.
Jafo ameyasema hayo
alipokuwa anafanya ziara yake katika hospitali ya Mvumi ambapo amezindua huduma
ya Hospitali Kimbizi inayohudumiwa na Madaktari Bingwa ambao watatoa huduma ya
kitabibu ndani ya siku tano kuanzia leo, tarehe 15 hadi Mei 19, 2017.
Madaktari hao bingwa
watatibu magonjwa ya ndani kwa watu wote, watoto, mifupa, masikio, pua na koo,
meno, upasuaji na magonjwa ya uzazi kwa upande wa akinamama.
Alisema katika sehemu
mbalimbali alizopita kumekuwa na changamoto ya kukosa huduma bora katika vituo
vya Afya kutokana na urasimu walionao Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za
Mitaa na kufanya Wananchi wengi wasio na uwezo wa kupata huduma hizo katika kipindi
cha nyuma na kwa kipindi hiki Serikali imeshatoa
ufumbuzi ambao Viongozi mnapaswa kuzitumia vyema pesa za Miradi ya Afya kama Busket
Fund katika kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi wote.
Aidha Jafo amewataka
Wananchi kushiriki kikamilifu katika kupata huduma hizo kutoka kwa Madaktari
bingwa waliotoka katika hospitali mbalimbali nchini kwani huduma hizo
zinapatikana kwa bei nafuu na kutoka kwa Madaktari bingwa wenye uzoefu mkubwa
na wa muda mrefu .
Amepongeza ushirikiano
uliopo wa Mganga Mkuu wa Dodoma Dk.James Kiologwe Mbunge wa Jimbo la Mtera, Mkuu
wa Wilaya ya Chamwino, wadau mbalimbali pamoja na Kanisa la Anglikana kwa kuweza
kuendesha zoezi hilo la huduma.
Akihitimisha hotuba
yake iliyojaa maelekezo ya Serikali, Jafo amesema baada ya zoezi hili
kukamilika ingependeza madaktari bingwa wote walioshiriki zoezi hili katika
Wilaya zote za Dodoma waje kujipongeza mjini Dodoma na kuwa mfano bora wa
kuigwa kwa kuwa zoezi hili ni zoezi la kwanza kufanyika nchini na likiwa
limefanyika mkoani Dodoma.
0 Comments