*Awasihi wananchi wote wanunue hisa kabla muda haujaisha
*Asema wajasiriamali, wakulima, wafugaji na wavuvi wana fursa sawa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amenunua hisa za kampuni ya Vodacom Tanzania Plc zenye thamani ya sh.
milioni 10 pamoja na nyingine za sh. milioni 10 kwa ajili ya mke wake,
Mary Majaliwa.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo
leo hii (Ijumaa, Mei 5, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari
mbele ya wakuu wa Masoko ya Hisa na Dhamana; Soko la Hisa la Dar es
Salaam, viongozi wa Baraza la Uwezeshaji na kampuni ya Vodacom katika
ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amewasihi Watanzania
walioko ndani na nje ya nchi wachangamkie fursa ya kununua hisa hizo ili
waweze kuwa wamiliki wa kampuni kupitia hisa zao. “Hii ni fursa kwa
Watanzania kumiliki kampuni. Ukinunua hisa, unashiriki kikamilifu
kumiliki kampuni na pia unaboresha uchumi wako binafsi. Ninawasihi
Watanzania wote tumieni fursa hii kununua hisa hizo kabla muda
haujaisha,” alisisitiza.
Alisema watumishi wa umma wamepewa
ya kununua hisa hizo kupitia mipango iliyowekwa na Makatibu Wakuu wao
lakini pia amewasihi viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi
wachangamkie fursa hiyo ili nchi iweze kupata kodi kupitia makampuni
hayo.
“Hii ni fursa kwa kila Mtanzania,
kwa viongozi kwa taasisi na mashirika ya umma, taasisi binafsi,
wajasiriamali wadogo kama akinamama lishe au madereva wa bodaboda.
Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) nao pia wanunue hisa kwani
watakuwa wanachangia uchumi wa nchi na wakati huo wanaweka akiba
nyumbani,” aliongeza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip
Mpango uwekezaji kwenye hisa ni njia mojawapo ya kuwawezesha Watanzania
kumiliki uchumi wa nchi.
“Huko mtaani ukisema uchumi wa
nchi unakua, watu wanabisha wakidai kuwa hawaoni unakua kwa sababu
hawana fedha mifukoni. Hii ni fursa nyingine ya kuwawezesha kukua
kiuchumi, ninaomba waichangamkie,” alisema.
Alisema sekta ya mawasiliano ni
miongoni mwa sekta inayokua kwa kasi hapa nchini kwani katika robo tatu
ya mwaka, sekta hiyo imekua kwa asilimia 11.3. “Niwasihi Watanzania
wenzangu, tununue hisa za Vodacom ili tuweze kuboresha uchumi wetu,”
alisema.
Alisema anatoa ombi maalum kwa
wafugaji kukubali kuuza mifugo yao na kununua hisa ili kupunguza idadi
ya mifugo yao, jambo ambalo alisema litapunguza migogoro baina yao na
wakulima.
“Wakulima wa vitunguu, alizeti,
maua au wafugaji wa samaki nao pia wanaweza kununua hisa na kuwa na
mitaji kwa ajili ya shughuli zao. Ninawasihi wote watumie fursa hii ili
kumiliki kampuni,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana, Bi. Nassama Masinda alisema
amefurahishwa kuona Waziri Mkuu akinunua hisa za kampuni ya Vodacom
katika soko la awali.
Alisema uuzwaji wa hisa hizo ni
utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha
Watanzania kuwa wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi hapa nchini.
“Marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta sura ya
306 yanazitaka kampuni za simu na mawasiliano ya kielektroniki kuuza si
chini ya asilimia 25 ya hisa zao kwa umma wa Tanzania kupitia masoko ya
mitaji (IPO).”
Alisema baada ya hapo hisa hizo
zinapaswa kuorodheshwa kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam baada ya
kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, sura ya 79.
Kampuni ya Vodacom ilitoa hisa milioni 560 kwa umma kwa bei ya sh. 850
kila moja na hivyo kutarajia kukusanya sh. bilioni 476.
Alisema hivi sasa, wawekezaji
kwenye masoko ya mitaji ni watu 500,000 tu ikilinganishwa na Kenya
ambayo ina wawekezaji milioni 1.7; Uganda (40,000) na Rwanda (14,000).
“Vodacom ina wateja milioni 6.2, iwapo nusu ya wateja wake wote
watashiriki ununuzi wa hisa, idadi ya wawekezaji kupitia masoko ya
mitaji na dhamana itaongezeka kwa asilimia 1,140. Na haya yatakuwa ni
mageuzi makubwa katika sekta ya masoko ya mitaji si hapa nchini tu bali
katika Afrika Mashariki,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Dodacom, Bw. Ian
Ferrao alisema mauzo ya hisa yanayofanywa na kampuni hiyo ni makubwa
mara nne ya mauzo ambayo yamewahi kufanyika hapa nchini.
Alisema kampuni hiyo ambayo
imekwishafanya kazi kwa miaka 17 hapa nchini, imewekeza zaidi ya sh.
trilioni mbili katika mtandao wa mawasiliano nchini Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 5, 2017.

0 Comments