Katibu wa Chama cha askari
wastaafu waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia(TLC) Mzee Sylvester
Lubala (katikati) akizungumza na waaandishi wa habari (hawapo pichani)
juu kumuunga mkono Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua katika vita ya
madawa ya kulevya pamoja na kupiga vita uhujumu uchumi nchini, kulia ni
Mwenyekiti wa Chama hicho Mzee Rashid Bakari na kushoto ni Mjumbe wa
chama hicho Mzee Damian Rashid.
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
CHAMA cha askari wastaafu
waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia(TLC) wamempongeza na kumuunga
mkono Rais Magufuli kwa hatua anazozichukua katika vita ya madawa ya
kulevya pamoja na kupiga vita uhujumu uchumi nchini.
Hayo yamesemwa leo na Katibu wa
chama hicho Mzee Sylvester Lubala wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu kuahirishwa kwa mkutano mkuu wa chama hicho uliokuwa
umepangwa kufanyika Juni 9 hadi 10 jijini Dar es Salaam.
“Chama cha Askari Wastaafu
waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia tunapenda kumpongeza Rais Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli kwa hatua sahihi aliyochukua ya kupiga vita
madawa ya kulevya ambayo yanawadhuru watoto na wajukuu wetu,” alisema
Mzee Lubala.
Aidha katika hatua nyingine wazee
hao wamemuomba Mhe. Rais Magufuli kuwasaidia kutatua kero mbalimbali
zinazowakuta hususani katika kupata huduma za afya kwani wamekuwa
wakisumbuliwa kutokana na kutokuwa na uwezo wa kifedha.
Pia wameishukuru serikali kwa
kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuwasaidia kuwaarifu wajumbe wa
chama hicho kote nchini kuhudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa viongozi
wa chama hicho Taifa.
Awali mkutano mkuu wa chama hicho
ulipangwa kufanyika Juni 9 hadi 10 lakini kutokana na mfungo wa Ramadhan
wamelazimika kuahirisha hadi Julai 8 na utafanyika jijini Dar es
Salaam.


0 Comments