Na
Robert Hokororo
Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Stephen Magoiga amesema
kuundwa kwa mfumo wa sekta za umma (PS3) utasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku
zinasimamiwa vizuri.
Amesema
mfumo huo pia utaleta tija katika vituo vya kutolea huduma na kusaidia
upatikanaji wa taarifa sahihi katika mahesabu ya mapato na matumizi ya halmashauri
nchini.
Magoiga
ametoa kauli hiyo wilayani hapa wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa uhasibu na
utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma (FFARS)
yaliyofanyika katika kata ya Maganzo.
Alisema
mafunzo hayo yaliyolenga waratibu elimu kata na watoa huduma katika vituo vya
afya yatawajengea uwezo wa kusimamia taarifa za matumizi ya fedha na
kuhakikisha zinatolewa kwa usahihi, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Nafahamu kwamba mafunzo haya yanafanyika sehemu mbalimbali nchini ili kuhakikisha
mnakuwa katika nafasi ya kwenda kuwafundisha watoa huduma kwenye vituo vya
kutolea huduma za elimu vikijumuisha zahanati, vituo vya afya, hospitali, shule
za sekondari na za msingi,” alifafanua.
Magoiga
aliongeza kuwa lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinakuwa na
mfumo maalumu wa kuandaa taarifa za mapato na matumizi hivyo kuchangia
uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alikiri
changamoto ya upatikanaji taarifa sahihi za fedha vituoni hivyo halmashauri
kushindwa kutoa taarifa sahihi za matumizi ya ruzuku zinazotolewa na wakati
mwingine kusababisha kupata hati ya mashaka kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG).
“Ukweli
ni kwamba hakukuwa na mfumo sahihi wa kusaidia kulizuia hilo lakini kwa mfumo
huu mpya sasa, utasaidia kuhakikisha kunakuwa na muundo maalum wa kuhifadhi
taarifa za mapato na matumizi, na hivyo kuongeza uwazi na uwajibikaji wa vituo hivyo
kupunguza changamoto zilizokuwepo awali,” alisema.
Aidha
mkurugenzi huyo aliagiza matumizi ya tovuti za mikoa na halmashauri katika
kuweka taarifa zote za mapato na matumizi ya fedha za umma ambayo ni maagizo ya
Serikali.
Mradi
huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) pamoja
na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wizara mama
zinazoshughulikia sekta za fedha, afya na elimu.









0 Comments