Na
Jonas Kamaleki
Kati ya mambo ambayo
yamekuwa yakimuumiza kichwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ni ukusanyaji
wa kodi hivyo juhudi za makusudi zimefanyika ili kutimiza azma hii.
Serikali ya Awamu ya
Tano imetekeleza ahadi yake kwa wananchi ya kuongeza pato la Taifa kwa
kukusanya kodi. Azma hii imetekelezwa kwa vitendo kwani mwanzoni mwa utawala wa Rais Magufuli mapato yatokanayo
na kodi yameongezeka kutoka takriban bilioni mia nane hadi kufikia trilioni 1.3
kwa mwezi.
Hivi karibuni, Rais
Magufuli amezindua Mfumo Mpya wa Ukusanyaji kodi kwa njia ya Kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS),
mfumo ambao unatarajiwa kuongeza mapato kwa kiwango kikubwa.
Akizindua Mfumo huo,
Rais Magufuli alitoa agizo kwa makampuni ya simu na kusema, “Nimepata taarifa
kuwa hadi sasa Kampuni za simu za TTCL, Hallotel na Smart ndizo pekee
zilizojisajili katika mfumo huu, sasa natoa wito kwa makampuni mengine na
mabenki yahakikishe yanasajisajili kabla ya mwezi Desemba mwaka huu”.
Ili kuwezesha mfumo
huo kufanya kazi, makampuni yote ya simu, mabenki na yale yanayofanya miamala
kwa njia ya kielektroniki yanapaswa kujisajili katika Kituo cha Taifa cha
Kuhifadhia Taarifa (Data Centre)
ambacho kina uwezo wakuona kila muamala unaofanyika na kufanya ukokotozi wa
kodi inayostahili kulipwa.
Mfumo huu kwa mujibu
wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, ni
sehemu ya mchakato wa ukusanyaji wa mapato unaojumuisha mifumo mbalimbali iliyowekwa
pamoja kuweza kufanya ukadiriaji, tathmini na ukokotozi wa kodi kutoka kwenye
miamala mbalimbali inayofanyika kielektroniki.
Ni Mfumo ambao
unahusisha moduli tisa zinazofanyakazi mwanzo hadi mwisho kuhakikisha kodi
inakusanywa, inakadiriwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka
ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar ambazo zipo Benki Kuu. Amezitaja
moduli hizo kuwa ni : moduli ya kukusanya taarifa, kutunza taarifa, kuhakiki
taarifa na kushirikisha mifumo. Moduli nyingine ni ya kuzuia udanganyifu, ya kukusanya kodi, ya kutoa ripoti, ya
usalama wa miundombinu na moduli ya kutoa taarifa kwa kinachotokea.
Bwana Kichere
anaeleza kuwa imekuwepo mifumo mingine ya kukusanya mapato kielektroniki ambayo
imeonyesha kuwa na mianya ya kukwepa kodi. Kuhusu mifumo mingine Kamishna Mkuu
anasema baadhi ya mifumo ambayo imeanzishwa na inatekelezwa kuanzia kipindi cha
mwaka 2012 ni kama ifuatavyo:
Electronic
Cargo Tracking System (ECTS). Mwaka 2012 Mamlaka
ya Mapato Tanzania iliunda mfumo kufuatilia mizigo ipitayo katika bandari ya
Dar es Salaam kuelekea nchi jirani.
Mfumo huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la ukwepaji wa kodi kwa
mizigo iliyokusudiwa kupelekwa nchi jirani
Mfumo wa
Kielektroniki wa ulipaji Kodi (Revenue Gateway System) ulianzishwa mwaka 2013
na unawasiliana na Benki Kuu pamoja na benki za kibiashara hivyo unamuwezesha
mlipakodi kufanya malipo ya kodi mbalimbali kupitia benki au kwa kutumia simu
ya kiganjani akiwa mahali popote na hivyo kuondoa usumbufu kwa mlipakodi. Pia
mfumo huu unawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za mapato ya Serikali kwa
wakati.
Mfumo wa
kielektroniki wa Forodha yaani Tanzania Customs Integrated System (TANCIS).
Mfumo huu ulianzishwa mwaka 2014 na unatumika kuthaminisha mizigo na kukadiria
kodi ili kodi sitahiki ilipwe pamoja na kuratibu shughuli za uondoshwaji mizigo
maeneo ya forodha. Mifumo hii yote imewezesha kuongeza mapato kutoka wastani wa
shilingi trilioni 3.4 mwaka 2013/14 hadi trilioni 5.2 kwa mwaka 2015/16.
Bwana Kichere
anafafanua kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) imegundua kwamba kuna mianya ya kimfumo inayoikosesha
serikali mapato kutoka kwa walipakodi mbalimbali.
Changamoto ni kubwa
zaidi kwenye huduma zitolewazo kwa mifumo ya kielektoniki ya makampuni ya simu
(Mobile Network Operators) ambapo wahusika hutoa huduma na kupata mapato yao
mara moja, wakati ambapo kodi (kodi yaongezeko la thamani – VAT na ushuru wa
bidhaa – (Excise Duty) inayopaswa kulipwa kwa serikali inategemea mawasilisho
ya makadirio kutoka kwa makampuni husika. Hali hiyo, husababisha baadhi ya
makampuni kutumia mwanya huo kuipunja serikali kodi stahiki.
Ili kukabiliana na
changamoto hizi, TRA na ZRB kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali
zimeunda mfumo utakaowezesha kutathmini, kukusanya na kuhasibu kodi kwa njia ya
kielektoniki moja kwa moja bila kuathiriwa na utashi wa mtu (without human
intervention).
Ndoto ya Rais
Magufuli ya kubuni vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato inaanza kutimia baada
ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2017/18 kuanisha vyanzo hivyo.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango akiwasilisha makadrio ya bajeti ya Serikali kwa
mwaka wa Fedha unaoanza Julai 1, 2017 anasema, “Serikali itatoza Kodi ya
Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na
Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum
(flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini
(50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
“Serikali itawatambua
rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika
maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya
kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika kwa kuwapatia
vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya”, alisema Dkt. Mpango.
Katika kutekeleza
suala la ukusanyaji wa mapato kielektroniki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi imezindua Mfumo wa kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa
njia ya kielektroniki. Mfumo huu umeonyesha kuwa ni bora katika kuongeza
ukusanyaji wa mapato.
Kwa Mfumo huo,
mlipaji kodi hahitaji kwenda Wizarani au kituo cha malipo kulipa kodi bali
anaweza kufanya hivyo akiwa mahali popote kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa
kupitia menyu kuu ya Taifa ambayo ni *152*00#. Njia hii itamwondelea mlipaji
usumbufu ikiwemo kupoteza muda mwingi kutoka napokaa na kufika Wizarani kwa
ajili ya kulipia kodi.
Mkuu wa Kitengo cha
Kodi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami ansema
kuwa katika kipindi kifupi tangu mfumo huo uanze kutumika, mapato yameongezeka
kwa shilingi milioni 9 ndani ya siku tano. Hii ni kutoka bilioni 2 hadi bilioni
2.9 kwa siku tano. Mwenendo huu wa ongezeko unaonyesha kuwa kwa mwezi hadi kwa
mwaka mapato yataongezeka kwa kiwango kikubwa.
Naye Mkurugenzi wa
Mifumo ya Kifedha wa Wizara ya Fedha na Mipango anasema kuwa kwa kutumia mfumo
huo mtu atatumiwa ujumbe wa majibu kuonyesha kiasi cha fedha alicholipia ambao
utahesabika kama risti.
Hakika mifumo hii
ikisimamiwa barabara, ni dhahiri kuwa changamoto za kibajeti zitapungua. Kulipa
kodi ni suala la msingi na ndiyo maana kwenye nukuu za Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu kodi zinasema, “Serikali ya wala rushwa
haiwezi kukusanya kodi”. Mwalimu alisisitiza ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya
maendeleo ya wananchi zikiwemo huduma za kijamii kama vile; elimu, afya, maji
safi na salama na miundombinu.
0 Comments