Na
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali imebuni vyanzo vingine vya mapato ili
kupanua wigo wa kodi kwa ajili ya maendeleo endelevu nchini na kukuza uchumi wa
Taifa.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha
2017/18 Bungeni mjini Dodoma, waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango
amesema kuwa Serikali itaendelea na
ukusanyaji wa kodi ya majengo (yaliyothaminiwa na yasiyothaminiwa) kwenye halmashauri
zote nchini.
Ameongeza kuwa jukumu hilo litasimamiwa na Wizara
ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Serikali itatoza Kodi
ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na
Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum
(flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini
(50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
“Serikali itawatambua rasmi wafanyabiashara wadogo
wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi mfano
mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga
mboga, ndizi, matunda, na kadhalika kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi
wanazozifanya”, alisema Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali
itaendelea kusimamia na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs)
kwenye Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na kwa wafanyabiashara.
Ili kudhibiti mapato yatokanayo na madini, Dkt.
Mpango amesema Serikali haitoruhusu usafirishaji wa madini kutoka migodini na
kupeleka moja kwa moja nje ya nchi. Aidha, Serikali itaanzisha maeneo maalum
(clearing houses) katika viwanja vya kimataifa, migodini, na kadhalika ambapo
madini hayo yatathibitishwa na kupewa kibali cha kusafirisha madini hayo
ambacho kitatozwa ada ya asilimia moja (clearing fee) ya thamani ya madini
hayo.
Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema Serikali
itafungua akaunti maalum (Escrow Account) kuanzia mwezi Julai 2017 ili
kurahisisha na kuhakikisha kwamba marejesho ya Ushuru wa Forodha wa ziada
(Additional Import Duty) wa asilimia 15 unaolipwa na waagizaji wa sukari ya
viwandani yanafanyika kwa wakati. Hatua hii itaiwezesha Mamlaka ya Mapato
kufanya marejesho kwa wakati kwa wazalishaji wanaotumia sukari hiyo katika
kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Dkt. Mpango amesititiza kuwa Serikali itaimarisha
mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki ili
kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali.
“Mfumo uitwao “Government e-payment Gateway
System” uko tayari kwa ajili ya matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali. Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia
mfumo huu”, alisema Dkt. Mpango.
Amebainisha pia kuwa Serikali imezindua mfumo mpya
wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System
(e-RCS)) ambao utadhibiti udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa
kushirikiana na walipa kodi katika kukadiria kodi sahihi. Aidha, mfumo huu
utawasaidia walipa kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi cha kodi wanayopaswa
kulipa.
Mfumo huo wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu wa fedha kwa
usimamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kwa upande wa Bara na Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) kwa upande wa Zanzibar.
Katika mwaka 2017/18, Serikali inapanga kutumia
jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni
19,712.4 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha shilingi
bilioni 7,205.8 za mishahara na shilingi bilioni 9,461.4 kwa ajili ya kulipia
deni la umma na huduma nyinginezo. Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa
shilingi bilioni 11,999.6 sawa na asilimia 38 ya bajeti.


0 Comments