Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Vijana Wazalendo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua alizozichukua kuwapinga
wanyonyaji wa uchumi na raslimali za nchi kupitia seta ya Nishati na
Madini.
Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wazalendo Tanzania, Bwana Mwita Nyarukururu alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
Bwana Mwita amesema ana hakika kuwa Watanzania wanafuatilia
juhudi za Mhe. Rais Magufuli katika sekta ya Nishati na Madini kwa
kuunda Tume ya wataalam mbalimbali kufanya uchunguzi na upembuzi
yakinifu katika madini.
“Wote tumeshuhudia ripoti ya wataalam wa madini chini ya
Mwenyekiti, Prof. Abdulkadir Mruma ambapo Tume imeeleza masikitiko yake
makubwa dhidi ya makampuni ya madini nchini yanavyokwapua na kusafirisha
raslimali zetu bila Taifa kunufaika”, alisema Mwita
Aidha, Mwita amesema kuwa unyonyaji na uhujumu uchumi katika
sekta ya madini umekuwa ukipigiwa kelele kwa takriban miaka 17 na wazee
pamoja na wananchi kwa ujumla juu ya tahadhari yao kwa Taifa kuwekeza
katika uzalishaji wa madini kutokana na mikataba kuwa ya siri na mibovu
isiyonufaisha wananchi.
Aidha wamemwomba Mhe. Rais kuvunja mikataba ambayo haina
maslahi kwa taifa bila kujali udogo au ukubwa wa kampuni hizo, ikiwa ni
pamoja na kupeleka Bungeni mikataba na sheria zote zinazohusu nishati na
madini kwa lengo la kujadiliwa upya kwa maslahi mapana ya Taifa .
Kwa upande wake, mjumbe wa Jukwaa la Wazalendo, Bi. Rose
Manumba amesema inashangaza kuona huduma za kijamii kama sekta ya Afya,
Elimu na Miundombinu zinazorota kwa kukosa fedha wakati matrililioni ya
fedha yanachukuliwa na wajanja wachache.
Amemuomba Mhe. Rais na wananchi kwa ujumla wasichoke katika
mapambano haya ya kukomesha wizi wa raslimali za Watanzania walizopewa
na Mungu.
“Kwa kweli tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii ili
nchi yetu na raslimali zake ziwe na manufaa kwa kizazi chetu na vizazi
vijavyo”, alisema Manumba.
Mwezi uliopita Mhe. Rais alipokea Ripoti ya uchunguzi wa
Makinikila ambayo ilionyesha kuwa tani za dhahabu na madini mengine
yenye thamani kubwa yalipatikana kwenye mchanga uliokuwa usafirishwe nje
ya nchi. Katika ripoti hiyo jumla ya takriban tani 15 za madini
zilikutwa kwenye makontena 277 ya makinikila yayozuiliwa kusafirishwa
nje na Mhe. Rais Magufuli, thamani yake inakadiriwa kuwa ni shilingi za
Kitanzania trililioni 1.3.
Kufuatia ripoti hiyo, uteuzi wa Waziri mwenye dhamna ya Nishati
na Madini, Prof. Sospiter Muhongo ulitenguliwa na Mhe. Rais, na
aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Madini Nchini, alisimamishwa kazi.
Juhudi hizi za Mhe. Rais katika kupambana na ufisadi nchini zimeungwa mkono na watanzania wengi wakiwemo viongozi wa dini.


0 Comments