Kaimu Mkurugenzi Mkuu
–TAWA Bw. Martin Loibooki akisoma risala mbele ya mgeni Rasmi
Na Mwandishi
wetu, Katavi
Wizara ya
Maliasili na utalii imewataka wadau wa uhifadhi kote nchini kuunga mkono mpango
wa Serikali wa kujenga mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji
kwenye pori la akiba la Selous ambao ukikamilika unatarajiwa kuzalisha zaidi ya
megawati 2,100.
Katibu Mkuu
wizara ya Maliasili na utalii Meja Jenerali Gaudance Milanzi amesema
utekelezaji wa mradi huo wa umeme ni wa muhimu kwa taifa kwani utasaidia
kuharakisha maendeleo ya taifa kuelekea azima yake ya Tanzania ya viwanda na
uchumi wa kati.
Akiongea wakati
akifunga mafunzo ya askari wa wanyamapaori kutoka Mamlaka ya wanayamapori
Tanzania -TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Katibu mkuu Meja Jenerali
Gudance Milanzi amesema mradi huo wa umeme pamoja na mradi wa bwawa la maji la
Kidunda utachukua eneo dogo tu la pori la akiba la Selou lenye ukubwa wa zaidi
ya kilomita za mraba elfu 50.
Amesema pori
hilo ndilo kubwa miongoni mwa mapori ya aina hiyo ulimwenguni na ukubwa wake ni
zaidi ya nchi za Rwanda na Burundi zikiunganishwa kwa pamoja.
Katibu Mkuu
amesema ujenzi wa miradi hiyo hauna tafsiri kwamba Tanzania haithamini masuala
ya uhifadhi bali unazingatia uhifadhi wenye manufaa kwa jamii na maendeleo ya
taifa na hasa dhamira ya serikali ya rais Dk John Pombe Magufuli kuelekea
Tanzania ya viwanda ambayo inahitaji nishati ya umeme itakayoyotosheleza
mahitaji ya taifa.
Amesema
Tanzania inatambua umuhimu wa uhifadhi ndiyo maana imetenga eneo la zaidi ya
asilimia 28 ya eneo lote la nchi kavu Tanzania bara kwaajili ya uhifadhi wa
aina mbalimbali ukiwemo wa wanayamapori na misitu ya vyanzo vya maji ambayo ni
muhimu kwa shughuli za kijamii na kiuchumi, “ ni nchi chache sana duniani zenye
eneo kubwa la uhifadhi kama Tanzania” alisisitiza katibu mkuu.
Katibu mkuu
amewataka wafanyakazi wa wizara na watanzania kwa ujumla kutokuwa kikwazo kwa
utekelezaji wa mradi huo na kwamba wadau wanaotaka kuisaidia Tanzania wasaidie
kuhakikisha inatumia maliasili zake kupiga hatua ya kimaendeleo ikiwemo misaada
ya teknolojia za kisasa na rafiki wa mazingira kusaidia kufikia malengo yake
kimaendeleo.
“Mtakumbuka mh.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli hivi karibuni
alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Pwani amezungumzia kwa kirefu sana
umuhimu wa miradi hiyo ukiwemo wa bwawa la Kidunda na wa umeme wa Stieglars
Gorge, sasa sisi kama wahifadhi na kama watumishi lazima tumuunge mkono na
tusiwe kikwazo katika dhamira hii njema” alisema Jenerali Milanzi’’.
Ametoa mfano wa
nchi ya Qatar ambayo amesema ilikuwa na eneo la uhifadhi lililokuwa kwenye
orodha ya maeneo ya urithi wa dunia kutokana na uwepo wa baadhi ya viumbe adimu
lakini walipogundua mafuta, waliamua kujitoa kwenye urithi wa dunia ili wachimbe
mafuta na kuinufaisha nchi hiyo na maendeleo ya wananchi wake.
Akizungumzia
kuhusu tatizo la mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, Katibu mkuu amewataka
wahifadhi kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo na kusimamia sheria
zilizotungwa na Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinakataza
mifugo kuingia hifadhini kinyume cha sheria.
Amesema ndiyo
maana serikali inatumia fedha nyingi kugharamia mafunzo ya askari wa
wanyamapori na wahifadhi ili kuwaongezea ujuzi na weledi wa kulinda maliasili za
taifa kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Katibu Mkuu
Meja Jenerali Gaudance Milanzi amezungumzia pia umuhimu wa kuhakikisha mapori
ya uhifadhi yanatumiwa kwa uhifadhi badala ya kutumika kwa mambo mengine
ikiwemo kilimo cha bangi na maficho ya majambazi na majangili na amewataka
wahifadhi na askari kushirikiana na vyombo vingene vya ulinzi na usalama
kuwafichua wahalifu wanaojificha kwenye mapori hayo na kufanya ujangili na
uhalifu mwingine.
Mapema katika
taarifa yake kwa katibu mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori
Tanzania -TAWA Martin Loibooki alieleza kuwa mafunzo hayo yamesaidia kuimarisha
uhifadhi kwenye mapori mbalimbali ya akiba nchini na maeneo ya uhifadhi wa
wanyamapori.
Aliwashukuru
wadau mbalimbali wa uhifadhi wa ndani na nje ya nchi wanaofadhili mafunzo hayo
na vitendea kazi juhudi ambazo amesema zimeanza kuzaa matunda ikiwemo
kuongezeka kwa idadi ya tembo na wanyamapori wengine kwenye mapori mengi
nchini.
Mfunzo hayo yaliyowashirikisha
askari wa wanyamapori wapatao 98 kutoka Mamlaka ya wanayamapori Tanzania TAWA
na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ni mwendelezo wa mafunzo yanayotolewa na Wizara
ya Maliasili na utalii kwa askari wa wanyamapori na watumishi wengine wa wizara
hiyo katika hatua za kuelekea mfumo wa jeshi usu.








0 Comments