Taharuki
imewakumba wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (Sia)
mkoani Mbeya na wananchi wanaofanya shughuli kando mwa barabara kuu ya
Tanzania -Zambia baada ya moto kuwaka ndani ya eneo la uwanja huo.
Moto
ambao chanzo chake bado hakijafahamika ulitokea jana mchana na kaimu
meneja wa uwanja huo, Jordan Mchami alisema iliwachukua takriban nusu
saa kuuzima.
Alipoulizwa
kuhusu cha moto huo Mchami alisema ulionekana kuanzia barabarani na
walipofuatilia kwa kuwauliza kina mama wanaofanya biashara ndogondogo
kando mwa barabara hiyo waliambiwa kuwa waliona lori lililokuwa
limeegeshwa eneo ulikoanzia hivyo wanahisi huenda mtu au watu waliokuwa
katika gari hilo walirusha kipande cha sigara na kusababisha nyasi
kuwaka.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga alipotafutwa kuzungumzia suala
hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema kamanda yupo kwenye
msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Hata
hivyo, taarifa za ofisa mmoja wa polisi aliyekuwapo eneo la tukio
ambaye aliomba jina lake lisiandikwe kwa kuwa si msemaji alisema, “Tumefanikiwa
kuuzima moto ambao ulienea eneo kubwa. Tunashukuru haukuweza kufika
maeneo ya kurukia ndege au kuharibu mali za uwanja huu.”
Uwanja
huo umeongeza wigo wa fursa za kibiashara na kurahisisha huduma za
usafiri wa anga kwa wakazi wa Mbeya, huku ukianza kuunganisha Kanda ya
Nyanda za Juu Kusini na maeneo mengine duniani.
Kadri
siku zinavyokwenda, watu kutoka nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Malawi wamekuwa wakiutumia uwanja huo.
Wageni
hao ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za biashara na utalii,
wamezidi kuifungua kibiashara mikoa ya Songwe na Mbeya na kuonyesha
ishara chanya kuwa uwanja huo unaelekea kuwa kitovu cha biashara kati ya
Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika.




0 Comments