Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) wilayani Kishapu wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku katika
kijiji cha Mwigumbi kata ya Mondo.
Sehemu ya
walengwa wa kaya maskini wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku kijij cha
Mwigumbi.
Na Robert Hokororo
Kaya 6019 katika halmashauri
ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, zinatarajia kunufaika na fedha sh.
milioni 204.6 zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF wilayani humo, Sospeter Nyamuhanga ofisini
kwake wakati akizungumzia zoezi la uhawilishaji fedha hizo linalotarajiwa kuvifikia
jumla ya vijiji 78.
Alisema kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Agosti 7 hadi
11 mwaka huo katika vijiji lengwa kwenye kata zilizo katika mpango wa TASAF III
wilayani humo .
Nyamuhanga alifafanua kwa kusema kuwa zoezi la uhawilishaji fedha kwa kaya
hizo linaanza kwa lengo la kuziwezesha kaya maskini ili zikwamuke kutoka hali ya
umaskini.
Mratibu huyo alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya
wanakaya 54 wameingizwa kwenye mpango huo wa TASAF III wakiwemo watoto
waliozaliwa katika kipindi hicho.
“Lengo la mpango wa TASAF ni kuhakikisha walengwa wanatimiza masharti kama
ya kuwapeleka watoto shule ili baadaye wapate elimu ambayo itawaondoa katika
umaskini na pia kuhakikisha wanawapeleka kwenye huduma za afya kupitia fedha
hizi,” alisema.
Mratibu huyo aliongeza kwa kubainisha kuwa mpango wa TASAF wilayani Kishapu
umeonesha mafanikio yakiwemo baadhi ya kaya kubadilika kimaisha kwa kufuga
mifugo kama ng’ombe na mbuzi.
Alisema kuwa baadhi ya walengwa tayari wamebadilisha aina za makazi yao
kutoka nyumba za tembe na nyasi na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali
inayoleta matumaini katika miradi kama hii.
Mratibu huyo amesema mfuko huo unatoa ruzuku za aina mbili, ya msingi
inayotolewa kwa kaya zote masikini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine
ni ya utimizaji masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa
kwenda shule na vituo vya kutolea huduma za afya
Aidha, Nyamuhanga aliwataka wanufaika
kuwa na matumizi sahihi ya fedha wanazopata ili lengo la TASAF la kuwatoa
katika umaskini na kuwafanya wajitegemee litime.
Kishapu ni miongoni mwa halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja
na Pemba zinazotekeleza Mpango wa TASAF III ili kuongeza kipato na fursa za
kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.



0 Comments