Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

Header Ads Widget

Ubinafisi Unavyo athiri Bwawa la Igombe na Kuwatesa Wakazi wa Tabora Mjini.

Na Tiganya Vincent RS-Tabora
UBINAFISI wa baadhi ya watu kupenda kujiangalia wenyewe zaidi kuliko wenzao na kupelekea kuendesha shughuli za kilimo hata kwenye vyanzo vya maji kunasababisha wakazi wa Manispaa ya Tabora kuanza kupata maji kwa mgao.

Ni katika hali hiyo ukipita katika kila mtaa wa Manispaa ya  Tabora kilio kikubwa ni mgao wa maji ambao umesababishwa na kupungua maji katika Bwawa la Igombe ambao ni tegemeo kubwa la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.

Tatizo hilo linaifanya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Tabora Mjini (TUWASA) kulazimika kusafisha maji yaliyojaa tope jingi kwa gharama kubwa ili kuhakikisha Wakazi wa Manispaa hiyo wanapata walau maji kidogo yaliyo katika hali safi na salama kwa ajili ya kulinda afya zao.

Hali hii inawafanya waandishi wa habari kwa kushirikiana na watendaji wa TUWASA kutembelea Bwawa hilo la Igombe ili kujionea hali halisi ya maji upungufu wa maji na uharibifu uliosababisha tatizo hilo hadi kufanya maji kupungua kwa mita 400 kutoka katika kingo zake hadi yalipo maji hivi sasa.

Kupungua huko kwa maji kumesababishia TUWASA kutumia gharama kubwa wakati wa uzalishaji wa maji yakiwa na tope jingi ukilinganisha na kipindi ambacho kinakuwa na maji mengi na tope ni kidogo.

Hatua hii inalenga kuhakikisha maji yanayosambazwa kwenye  maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Tabora yawe safi na salama ili kuewaepusha kupata magonjwa yanayotokana na maji kama vile homa ya matumbo na kipindupindu.

Kwa mujibu wa Meneja wa Biashara wa TUWASA Bernard Biswalo anasema kuwa maji yakiwa mengi ndani ya Bwawa la Igombe wanatumia jumla ya shilingi milioni 58 kwa mwezi kwa ajili ya kununua dawa za kuondoa tope  na kuua wadudu kwenye maji ambapo shilingi milioni 50 ni kwa ajili ya kuondoa tope na milioni 8 kwa ajili ya kuua wadudu walipo ndani ya maji ili kulinda afya za wateja wao.

Anasema baada ya kina cha maji kushuka ,hivi sasa wanalaziika kutumia kiasi cha milioni 103 kwa mwezi kwa ajili ya kununua dawa za kuondoa tope na kuua wadudu kwenye maji, ambapo milioni 95 ni kwa ajili ya kuondoa tope na milioni 8 kuua wadudu katika maji.

Fedha hizo zinafanya TUWASA iwe na ongezeko la shilingi milioni 45 katika fedha walizokuwa wakizitumia katika ununuzi wa dawa za kuua wadudu na zile za kuondoa tope kutoka zile za awali walizokuwa wakitumia katika kuhakikisha maji yanawafika wateja wao waliopo katika Manispaa ya Tabora yakiwa safi na salama.

Biswalo anaongeza kuwa kiasi hicho cha matumizi hayo ya fedha ni nje ya gharama ambazo TUWASA inazitoa kwa ajili ya huduma za umeme kwa ajili uzalishaji na usambazaji wa maji ambazo zinaanzia milioni 75 hadi 90 kwa mwezi.

Anasema kuwa licha ya TUWASA kutumia gharama kubwa katika uzalishaji wa maji imeendelea kutoa huduma kwa wateja wake kwa ile ile bila kuongeza hata senti moja.

Katika vibanda ya umma(public centre) ,ndoo yenye ujazo wa lita 20 Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Tabora Mjini imekuwa ikitoza shilingi 20 na kwa wale wanaotumia kuanzia Unit moja hadi chini ya 10 wamekuwa wakitozwa shilingi 920/- na wale wanazidi 10 na kuendelea hadi kufikia 15 wamekuwa wakitozwa shilingi 1800/-
Anaeleza kuwa licha ya msimu uliopita kuwa na upungufu wa mvua , sababu nyingine zilizosababisha upungufu wa maji katika bwawa hilo ni baadhi ya watu wanaondesha  shughuli za kilimo za mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga kama vile bamia, nyanya, matembele, mchicha matango na mahindi pembezoni mwake na maeneo jirani yake ambao utumia maji hayo katika umwagiliaji.

Biswalo anaongeza kuwa Bwawa hilo linategemea maji ya mvua kutoka katika Wilaya za Nzega na Igunga na hivyo baada ya baadhi ya watu kuanzisha kilimo cha mpunga mikondo ya kupeleka maji katika Bwawa la Igombe kwa kuiziba na kusababisha kuingia maji machache kuliko walivyokusudia.

Anasema wakulima hao wamekuwa wakijenga matuta ya majaruba ya Mpunga ambayo yazuia maji mvua kusafiri kuelekea katika Bwawa la Igombe ili TUWASA hatimaye iweze kuyatayarisha kwa ajili ya matumzi mbalimbali ya wakazi wa Manispaa ya Tabora.

Uchunguzi ulifanywa timu ya waandishi wa habari na watalaamu wa TUWASA waliotembelea Bwawa la Igombe uligundua kuwa kina cha maji kimeshuka sana kutoka urefu wa futi 5 ambazo zilipaswa kuwepo na kuwa futi 2 na kulifanya liwe na jingi kuliko maji.

Uwepo wa tope jingi katika Bwawani hapo umesababisha ugumu kwa Mamlaka hiyo kutoa huduma ya maji kwa wingi kwa wateja wake na hali hiyo imefanya kazi za kuhakikisha inazalisha maji safi na salama kuwa ngumu zaidi.

“Upunguaji wa maji katika Bwawa la Igombe umesababishia Mamlaka yetu ugumu wa kutoa huduma ya maji kwa wananchi kama walivyokuwa wamezoea… hata maji tunayotoa hivi sasa yanatoka  katika mazingira magumu na kwa kutumia gharama kubwa kuliko maji yalivyokuwa mengi bwawani”anasema Biswalo.

Anasema uangavu katika maji –NTU- (kiwango cha tope ) umeongezeka kutoka wastani ambao ulipaswa kuwepo wa 30 hadi 50 wakati maji mengi nakufikia NTU 300 jambo linawafanya TUWASA kutumia dawa za hali ya juu kuondoa tope katika maji.

“Hivi sasa tunalazimika kutoa maji kwa gharama kubwa ili maji yawe safi na salama na wananchi waweze kuyatumia bila kupata matatizo yanayotokana na maji” anaongeza Meneja huyo wa Biashara.

Anapendekeza hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuwaondoa wakulima wote na kubomoa matuta waliojenga katika njia za maji ambayo yanatoka katika wilaya za Igunga na Nzega ili pindi mvua zitakapoanza kunyesha maji yaingie kwa wingi na kuanza uzalishaji kwa wingi.

Biswalo anasema jambo hilo litafanikiwa iwapo kutakuwepo na ushirikiano wa pamoja kuanzia kwa viongozi wa vijiji ambapo njia za maji yaingia Igombe zinapitia na viongozi wengine wa Wilaya ya Mkoa ili kunusuru maisha ya wakazi wa Manispaa ya Tabora wasiathirike na ukosefu wa maji.

Anasema kuwa wakati wakazi wa Manispaa ya Tabora wakisubiri mradi wa maji ya Ziwa Victoria kwa kipindi cha miezi 30 ijayo ni vema hatua za muda mfupi zikachukuliwa katika kunusuru Bwawa hilo ili mvua ikinyesha maji yaingie kwa wingi
Mmoja wa Wakazi wa Ipuli katika Manispaa ya Tabora Agrikola Daudi anasema kuwa hali ilivyo hivi sasa katika Bwawa hilo hakuna jinsi wakazi wa  Tabora Mjini watakavyoweza kuepuka mgao wa maji kwani maji yalipo hapo ni kama tope pekee.

Anaongeza jambo la msingi ni kuwa wavumilivu na kutumia maji machache wanayopata vizuri kwa kubana matumzi katika maeneo mengine ambayo sio lazima utumie kwa uangalifu.

Daudi anasema kuwa tatizo hilo la mgao linaweza kudumu kwa mwezi wa Septemba na pindi mvua zitakapoanza kati ya Mwezi wa Oktoba kama ikiwahi au Novemba maisha yatarudi kama kawaida.

Hata hivyo viongozi mbalimbali kwa kutambua umhimu wa Bwawa hilo kwa mahitaji ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Tabora wamekuwa wakiendesha operesheni mbalimbali za kuwaondoa wavamizi ambao uendesha kilimo cha mboga mboga na matunda katika maeneo yanayozunguka na kusababisha upungufu wa maji.

Moja ya juhudi hizo ni wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tabora kwa kushirikiana na TUWASA mwezi uliopita ilipovamia eneo la Bwawa hilo na kuendesha oporesheni ya kung’oa mazao mbalimbali ya bustani yaliyokuwa yamepandwa na wavamizi katika eneo la Bwawa la Igombe.

Oporesheni hiyo iliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Queen Mlozi maji na kufanikiwa kung’oa zaidi za heka kumi za bustani zilizokuwa zimelimwa kando kando ya Bwawa la Igombe kwa lengoa kuzuia uharibifu huo kuendelea.

Baada ya Operesheni hiyo Mkuu huyo wa Wilaya anasema kuwa wavamizi hao ambao wanaendesha shughuli mbalimbali katika Bwawa hilo ikiwemo kilimo cha mboga mboga na wakati mwingine wamekuwa wakiweka dawa ambazo wakati mwingine zimekuwa zikiingia katika maji hayo ambayo ndio  tegemeo kubwa la wakazi wa Wilaya ya Tabora.


Mlozi anawashauri TUWASA wakawa wanatembelea eneo hilo la Bwawa ili kuhakikisha wanazuia ulimaji katika eneo hilo katika hatua za awali badala ya kugonja hali mazao yanakuwa ndio wanakwenda katika eneo hilo kuanza kung’oa.


Vitendo vya uvamizi vya vyanzo wa maji imekuwa ni ajenda kubwa ya Mkuu wa Tabora Aggrey Mwanri katika mikutano yake amekuwa akiwasisitiza Wakuu wa Wilaya na watendaji wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanawaondoa wavamizi wote katika vyanzo vya maji.

Anasema kuwa tatizo la kupungua kwa maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Bwawa la Igombe limetokana na watu kushindwa kusimama katika nafasi zao na kuwaacha watu wanakata miti ovyo kwa sababu ya uchomaji wa mkaa , ukaushaji wa tumbaku , mifugo kuwa mingi katika eneo moja na kilimo cha kuhama hama.

Bw. Mwanri anasema kuwa njia pekee ya kuhakikisha upungufu wa maji unaondoka katika maeneo mengi ambayo zamani yalikuwa na maji ya kutosha ni pamoja na kupanda miti kwa wingi katika maeneo ambayo hayana miti na kusimamia sheria kuwazuia watu wanaokata miti ovyo.

Anasisitiza kuwa wakazi wa maeneo mengine kama vile Kaliua , Urambo, Uyui na Sikonge wasipotia sheria na kuendelea na tabia yao ya ukataji miti ovyo kisha wanaichoma ipo siku maeneo hayo nayo yatakuwa kama ilivyo Wilaya ya Nzega na Tabora.

Mkoa wa Tabora hivi sasa unapata wastani wa milimita 600 za mvua wakati siku za nyuma ilikuwa ikipata wastani wa milimita 1600 na kufanya mabonde mengi kuwa na maji ya kutosha na hivyo kutokuwepo kwa tatizo kama ilivyo hivi sasa.

Mkazi wa maeneo ya Mwinyi katika Manispaa ya Tabora Zubeda Mwenya anaiomba Serikali ihakikishe mkandarasi anajenga mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria anafanya haraka ili awanusuru na mateso ya maji wanayopata kutokana na mgao uliosababishwa na upungufu wa maji katika Bwawa la Igombe.

Anasema kuwa hivi sasa wanalazimika kutafuta maji yasiyo safi na salama katika maeneo ya mbuga kwa ajili ya matumizi yao kila siku na kuongeza kuwa wakinamama ndio wanaoteseka sana na mgao.

Kwa upande wa Mkazi wa Ujiji katika Manispaa ya Tabora Monica Jeremia anasema njia pekee ya kuondoa tatizo ni kuitikia agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo pia linasimiwa vizuri na Mkuu wa Mkoa wa Tabora upandaji miti kwa wingia na kupambana na wale wanakata ovyo na kusihi katika vyanzo vya maji.

Anasema kuwa hata kama maji ya Ziwa Victoria yakija Tabora kama hawatajenga utamaduni wa kupanda miti na kulinda mistu ipo siku hata hayo yatakuwa machache kulingana na watu wanavyozidi kuongezeka.

“Njia ya pekee tumuunge Mkuu wetu wa Mkoa wa kupanda miti  na matokeo yake tutaanza kuyaona hata kabla ya maji ya Ziwa Victoria hayajafika” anasisitiza Monica.

Naye Mkazi wa Mihogoni katika Manispaa ya Tabora Salima Ally anatoa wito kwa viongozi kuwaondoa watu waliojenga majaruba yao katika mkondo wa maji ambao unapeleka maji katika Bwawa la Igombe ili kuwaondolea adha wakazi wa Manispaa ya Tabora ambayo wanapata ya kutumia maji machafu.

Anaongeza kuwa wenyewe wanapotumia eneo la kupitishia maji wanaoathirika ni wakinamama na watoto wanaotumia mwingi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia.

Post a Comment

0 Comments