Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Wakuu wa Shule (hawapo
pichani) wakati wa kufunga mafunzo yao ya siku mbili yaliyofanyika Mjini
Bariadi, (kulia) Afisa Elimu Mkoa, Mwl.Julius Nestory.
Baadhi
ya Wakuu wa Shule za Sekondari Mkoani Simiyu wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo,
Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani)alipozungumza nao wakati akifunga mafunzo ya siku
mbili Mjini Bariadi.
Na Stella
Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewataka
Wakuu wa Shule mkoani humo kuongeza ubunifu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika
shule zao.
Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga
mafunzo ya siku mbili kwa wakuu wa shule zote za Sekondari yaliyofanyika Mjini
Bariadi katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi
Amesema wakuu wa shule wanatakiwa kuwa wabunifu
hususani katika mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuwaandaa vizuri kitaaluma
wanafunzi ikiwa ni pamoja na mazoezi na mitihani ya kujipima ya mara kwa mara,
zitasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na kitaifa.
“Kiongozi lazima
uwe mbunifu, Mkiwa wabunifu kwenye shule watoto watafanya vizuri,mnapaswa
kubuni mbinu na mikakati mbalimbali kwenye majaribio ya darasani, mitihani ya
kujipima na kubuni namna ya kuwapa
motisha walimu wenu wapende kazi na kujiona ni wanafamilia katika shule
mlizopo” amesema Mtaka.
Aidha, amewataka
wakuu hao wa shule kujiwekea utaratibu wa kupita mara kwa mara madarasani kukagua
kwa lengo la kujiridhisha, ikiwa walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha
wanafunzi kama inavyotakiwa badala ya kusubiri kuletewa taarifa.
Mkuu huyo wa
Mkoa pia amewaasa wakuu hao wa shule kuwa na uongozi shirikishi ambao unajali
pande zote kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi ili waweze kujua kero na
masuala mbalimbali yasiyowaridhisha na waweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu
wa taratibu kuyapatia suluhu.
Vile vile Mtaka
amesisitiza wakuu wa shule kufanya vikao na wazazi kwa kuwa wazazi wanayo
nafasi kubwa ya kuchangia wanafunzi kufanya vizuri, hivyo akawataka wavitumie
vikao kupata maoni ya wazazi katika masuala mbalimbali ya kuboresha maendeleo
ya wanafunzi kitaaluma.
Sanjali na hilo
amewataka Wakuu hao wa Shule kuzingatia sheria, kanuni , taratibu na kuchukua
hatua stahiki pale inapobidi ikiwa ni pamoja na kutowaruhusu wanafunzi
wajawazito au waliojifungua kuendelea na masomo.
Kwa upande wake
Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius Nestory amesema katika mafunzo hayo
ya siku mbili wakuu wa shule wameelimishwa juu ya sheria zote nne za Elimu,
falsafa,nyaraka,kanuni mbalimbali za Elimu na sera mpya ya Elimu.
Nestory
amebainisha pia kuwa wakuu wa shule hao
wamepewa mafunzo ya utunzaji wa nyaraka za Serikali, udhibiti wa vitendo vya
rushwa, kusimamia shule na taaluma pamoja na utunzaji wa takwimu sahihi ambapo
amewataka wakuu wa shule hao kutumia sheria zilizopo katika kusimamia shule
kupitia mipango thabiti itakayotoa matokeo chanya.
Naye Magebu
Bugacha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwantimba ameshukuru uongozi wa Mkoa kuona
umuhimu wa kuwaandalia wakuu wa shule mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo ambayo yatawasaidia
na kuwapa uzoefu katika kuendesha na kusimamia shule zao.
Akitoa shukrani
kwa niaba ya Maafisa Elimu wa Wilaya za Mkoa huo, Afisa Elimu wa Wilaya ya
Meatu, Mwl.Estomia Makyara amesema maelekezo yote ya Mkuu wa Mkoa aliyoyatoa
wakati akifunga mafunzo hayo kwa Wakuu wa shule yatatekelezwa kwa uadilifu, ili
mkoa wa Simiyu uwe ni miongoni mwa mikoa mitatu bora kwa ufaulu katika mitihani
ya Kitaifa.
Jumla ya Wakuu
wa shule 152 kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu wamepata mafunzo hayo ambayo yalilenga kuwajengea uwezo
katika usimamizi na uendeshaji wa shule za Sekondari.


0 Comments