Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa mwenye kofia ya njano akiwa
katika majukumu ya ukaguzi wa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala-Vigwaza
inayojengwa mkoani Pwani.
Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto),
akifafanua jambo wakati akikagua mchoro wa Bandari kavu ya Kwala –Vigwaza
Mkoani Pwani.
Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa
maelekezo kwa Eng. Charles Salu Ogare anayesimamia ujenzi wa bandari kavu ya
Kwala-Vigwaza Mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Eng. Deusdedit Kakoko akifafanua jambo kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo
ya ujenzi wa bandari kavu ya Kwala –Vigwaza Mkoani Pwani.
Muonekano wa bandari
kavu inayojengwa na mkandarasi Suma-KJT katika eneo la Kwala-Vigwaza
inayotarajiwa kuanza kutumika Januari mwakani ikiwa katika hatua mbalimbali za
ujenzi.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na
kasi ya ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Kwala Vigwaza Mkoani Pwani na
kumtaka mkandarasi Suma JKT kuongeza kasi na kuzingatia ubora.
Akizungumza mara baada
ya kukagua ujenzi huo ameiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kushirikiana
na Shirika la Reli Tanzania (TRL) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS)
kuhakikisha wanaunganisha kwa haraka ili reli na barabara zinazoingia katika
bandari kavu hiyo zinakamilika na hivyo kuiwezesha bandari kavu hiyo kuanza
kutumika ifikapo Januari mwakani.
“TPA, TRL na TANROADS
uzuri wote mko kwenye wizara moja shirikianeni na hakikisheni kilomita 15 za
barabara inayoingia kwenye bandari kavu hii na kilomita moja ya reli zinajengwa
haraka,” Amesema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko kuhakikisha ujenzi wa bandari kavu
ya Kwala-Vigwaza unazingatia ubora na viwango vilivyopo katika mkataba ili
kuiwezesha kuhudumia zaidi ya makontena milioni moja kwa mwaka na hivyo
kupunguza msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Hakikisheni eneo la
bandari kavu linakuwa na maegesho ya kutosha, taa, maji ya uhakika, gari la
zimamoto, uzio na mashine ya ukaguzi wa mizigo scanner itakayowezesha kupima kila mzigo unaopandishwa na kushushwa
katika eneo hili,” amesisitiza Profesa Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu
wa TPA Eng. Kakoko amesema TPA imejipanga kuhakikisha ujenzi huo unatumia
gharama nafuu na mifumo yote ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA
inakuwepo katika bandari hiyo ili kuiwezesaha kufanya kazi kisasa na kwa
ufanisi zaidi.
“Tukifanikiwa kuhamia
hapa mzigo uliokuwa unasafirishwa kwa siku saba sasa utatumia siku tatu kufika Mwanza
hali itakayovutia wasafirishaji wengi kutumia bandari ya Dar es Salaam na hivyo
kukuza uchumi wa nchi na kuibua fursa za ajira,” amesema Eng. Kakoko.
Bandari Kavu ya Kwala
–Vigwaza inayojengwa na Mkandarasi SUMA JKT ambapo takribani kiasi cha shilingi
bilioni 9 kinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ili kuboresha huduma za
usafirishaji katika bandari ya Dar es Saalaam ambapo zaidi ya hekta 500
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo ambapo kwa kuanza hekta 120 sawa asilimia 24
zinajengwa katika awamu ya kwanza.
Imetolewa na kitengo
cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
0 Comments