Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2017.
Akiwasilisha
Bungeni Muswada huo leo Mjini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Katiba na
Sheria Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema kuwa lengo la
marekebisho yaliyopendekezwa ni kuboresha utekelezaji wa Sheria hizo kwa
kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia sheria hizo na kuongeza
masharti mengine ili kuleta uwiano kati ya Sheria zilizorekebishwa na
sheria zilizopo.
"Muswada wa Mabadiliko ya
Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2017 unapendekeza kufanya marekebisho
katika sheria 11 na kufuta sheria moja" amefafanua Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
Aidha, Masaju amesema kuwa
masuala muhimu yaliyozingatiwa katika Muswada huo ni pamoja na
kubadilisha vifungu vya Sheria kwa kufuta baadhi ya vifungu vya sheria
hizo na kuviandika upya, kufuta baadhi ya maneno kwenye vifungu vya
sheria, kuzingatia maneno mapya, kuongeza vifungu vipya na kufuta sheria
moja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya
kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mohamed Mchengerwa amesema kuwa
Kamati inashauri Serikali kuhakikisha Kamati maalumu ya kumshauri
Waziri kuhusu misamaha ya kodi iundwe na wataalamu waliobobea kutoka
katika fani na maeneo tofauti tofauti ili kujenga uwezo wa kamati hiyo
katika kumshauri Waziri husika kuhusu misamaha hiyo ya kodi.
Nae
Ally Saleh Ally kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Katiba na Sheria amesema kuwa kambi hiyo inashauri kuwa
haitoshi kuifuta RUBADA pekee bali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu
malalamiko ya wananchi wanaoituhumu kupora ardhi na hatua stahiki kwa
wote waliohusika zichukuliwe.

0 Comments