Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Suleiman
Jaffo akiongea na wajumbe wa Mkutano wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kutoka
Tanzania na Afrika Kusini walipokuwa ziarani Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Wa
kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia ni
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Serikalini
Bi. Plumla Williams akitoa neno kwa niaba ya wajumbe kutoka Afrika Kusini
walipotembelea maeneo ya ukombozi yaliyopo Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma ikiwa
ni sehemu ya agenda ya Mkutano kuhusu utekelezaji wa Programu ya Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika.
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Suleiman Jaffo (wa pili kushoto) akisalimiana na Mkurungenzi Mkuu
wa Kazi za Umma kutoka Afrika Kusini Bw. Mziwonke Dlabantu (kulia). Wa kwanza
kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi.
Baadhi ya Viongozi
kutoka Afrika Kusini wakiangalia makaburi ya Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini yaliopo
Wilayani Kongwa, Dodoma.
(Picha na Eleuteri
Mangi, WHUSM, Dodoma)
....
Na Bearice
Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Naibu Waziri Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Suleiman Jaffo amesema kuwa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa
Bara la Afrika (ALHP) una historia adhim kati ya Tanzania na Afrika Kusini na itasaidia
kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Mhe. Jaffo ameyasema hayo
leo Wilayani Kongwa, Dodoma wakati wa ziara ya Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na
Watalamu wa Programu hiyo kutoka Tanzania na Afrika Kusini kujionea maeneo yaliyotumika wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika
Kusini.
“Nchi ya Tanzania na
Afrika Kusini zina urafiki mkubwa na wa karibu kuliko nchi nyingine yeyote Afrika,
hivyo kupitia Programu hii tutazidi kuimarisha udugu na uhusiano uliopo”
amefafanua Mhe. Jaffo.
Ziara hiyo ilihusisha
maeneo ya makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini, Kambi walipokuwa
wanaishi, mahandaki walipokuwa wanajihifadhi dhidi ya maadui pamoja na madarasa
yaliyotumika kwa ajili ya mafunzo kwa wapigania uhuru.
Akizungumzia ziara
hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante
Ole Gabriel amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuona maeneo yaliyotumika
wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika Kusini na kujadili jinsi ya
kutunza maeneo hayo kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, Prof. Elisante
ameongeza kuwa ziara hiyo ina umuhimu kwa nchi zote ikizingatiwa Tanzania ndio
ilikuwa kinara wakati wote wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika hatua inayopelekea kuthamini
mchango uliotolewa na Tanzania kwa kusaidia kwa hali na mali katika ukombozi wa
wananchi wa Afrika Kusini.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa viongozi waliokuwepo
katika ziara hiyo kutoka Afrika Kusini kuona umuhimu wa maeneo hayo ya
kumbukumbu ya historia ya nchi yao kwa kuyatunza na kuyaendeleza kwa ajili ya
vizazi vijavyo ili watambue mchango wa Watanzania katika Ukombozi wa Bara la
Afrika.
Akiongea kwa niaba ya
viongozi kutoka Afrika Kusini, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Serikalini
Plumla Williams ameametoa wito kwa Serikali zote mbili kuwa suala la Ukombozi
wa Afrika lifundhishwe shuleni ili kuweza kutunza na kuimarisha Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika.
Mbali na hayo Bi.
Plumla kwa niaba ya Serikali ya Afrika Kusini ameahidi kuwa wataendeleza kasi
ya utekelezaji wa programu hiyo ili uweze kuwa na tija kwa pande zote mbili.
Programu ya Urithi wa
Ukombozi wa Bara la Afrika ina wajibu wa kukusanya, kuweka kumbukumbu,
kuhifadhi na kukumbuka nakishi ya Urithi wa Afrika tangu harakati za kupigania
Uhuru wa Afrika hadi Bara zima lililokombolewa.
No comments:
Post a Comment