Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King akisisitiza jambo wakati wa
ziara ya Kamati ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa TTCL kwenye kijiji
cha Sanga Itinje kilichopo Kata ya Itinje wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Kushoto kwa Mwenyekiti ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng.
Peter Ulanga
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Bwana John Mongella akiongea kuhusu mchango wa mifumo ya mawasiliano katika
kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali mbele ya Kamati ya Bunge ya
Miundombinu na watendaji wa kampuni za simu wa mkoani Mwanza (hawapo pichani)
wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na
upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini mkoani Mwanza. Aliyeketi ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King.
Meneja wa TTCL mkoa wa
Shinyanga Bwana Abdallah Lugage akitoa taarifa kwa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji
cha Sanga Intinje kilichopo kata ya Intinje wilaya ya Meatu mkoani Simiyu. Wa
tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Prof. Norman Sigalla King.
Wajumbe wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu, watendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, wafanyakazi
wa TTCL na wanakijiji wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ziara ya Kamati
hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnara wa kampuni hiyo kwenye kijiji cha
Sanga Intinje kata ya Intinje iliyopo wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
..
Serikali ya Awamu ya
Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. John Pombe
Magufuli imesisitiza kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi kwa
ujumla kulipa kodi kwa wakati ili nchi iweze kuongeza mapato yake kwa lengo la
kukuza uchumi, kujenga miundombinu ya barabara, reli, bandari, mawasiliano,
kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuweza kuwatumika wananchi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigalla wakati wa ziara ya
Kamati yake ya kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za
mawasiliano vijijini na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibishara kwenye mikoa
ya kanda ya ziwa ya Mwanza na Mara ambapo Serikali imetoa ruzuku kwa makampuni
ya simu za mkononi ili ziweze kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi kupitia
Mfuko wa Mawasiliao kwa Wote (UCSAF) ulio chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano.
Ameongeza kuwa Kamati
yake inasimamia sekta ya miundombinu yote nchini ikiwa ni pamoja na miundombinu
ya mawasiliano ambayo inategemewa na Serikali katika kukuza uchumi na
kuiwezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati na kuwa nchi ya viwanda. Prof.
Norman Sigalla King amesema kuwa miundombinu na huduma za mawasiliano ni moja
ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi, inachochea maendeleo ya taifa letu na kuiwezesha Serikali
kuhudumia wananchi wake kwa haraka, wakati, kwa ufanisi na kupunguza gharama za
Serikali kuwahudumia wananchi na kuokoa muda.
“Serikali imepeleka fedha nyingi
kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya nchi yetu kupitia Wizara hii kwenye
bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 ili nchi iweze kusonga
mbele”, amesema Prof. Norman Sigalla King.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza Bwana John Mongela ameieleza Kamati hiyo kuwa mifumo ya mawasiliano
imeiwezesha Serikali ya Mkoa wake kuongeza makusanyo ya mapato katika
Halmashauri za mkoa huo kutoka chini ya asilimia 46 kwa mwaka wa fedha uliopita
na kufikia asilimia 70 kwa mwaka huu wa fedha ambapo Halmashauri hizo zinatumia
zaidi ya asilimia 70 ya makusanyo hayo kuendesha miradi ya maendeleo na
kutekeleza majukumu mengine ya mkoa.
“Suala la mawasiliano duniani popote pale
ni nyeti sana kwa kuwa shughuli zote zinafanywa na mawasiliano kama vile
miamala ya kifedha, ulinzi na usalama wa raia na mali zake ambapo katika ngazi
ya Mkoa tumedhibiti kwa kiwango kikubwa ulinzi na usalama wa raia wetu na hali
ya mawasiliano kwenye mkoa wetu ni nzuri na tuna Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano,” amesema Mongella.
Ameongeza kuwa Mkoa huu ni mkoa wa pili kwa
ukubwa wa idadi ya watu na ni mkoa wa pili ambao unaongoza kwa kuchangia kwa kiasi
kikubwa mapato na ukuaji wa uchumi wa taifa letu.
Naye Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi
ili kufikisha huduma za mawasiliano kwenye mikoa ya kanda ya ziwa na visiwa vyake
takribani 36 vilivyopo kwenye kanda hii ili waweze kutumia mawasiliano kwa
ajili ya ulinzi na usalama na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza
kuwa kupitia Halotel, UCSAF imepeleka mawasiliano kwenye vijiji 78 vilivyopo
kanda ya ziwa na ziara hii inatusaidia kupata maoni ya wadau na kukusanya
changamoto ambazo zitasaidia kuboresha jukumu la UCSAF la kufikisha huduma za
mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara nchini nzima.
Mtaalamu wa
miundombinu wa kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana
Emmanuel Masanja amesema kuwa kampuni yao inajenga minara kwa kukodisha au kupewa
ardhi na mamlaka za serikali za vijiji kwa ajili ya ujenzi wa minara hivyo wanaishukuru
Serikali kuwapatia ruzuku ya kufikisha mawasiliano vijijini. Ameongeza kuwa
baadhi wa watu wanazuia maendeleo ya ujenzi wa minara kwenye baadhi ya maeneo
vijijini ambapo yanasababisha migogoro ambayo inachukua muda mrefu kukamilishwa
hivyo kuchelewesha ujenzi wa minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Bwana Masanja amesema
kuwa kampuni yao wanaiomba Serikali iwasaidie kusimamia upatikanaji wa ardhi
kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano kwenye ngazi ya Halmashauri zote
nchi nzima ili kuwawezesha wakandarasi kujenga minara kwa wakati ili kuharakisha
jitahada za Serikali ya Awamu ya Tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijiji
vyote nchi nzima na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara.
Aidha Mkurugenzi wa
Kanda ya Ziwa wa kampuni ya TIGO Bwana Ally Maswanya ameishukuru Serikali kwa
kuwapatia ruzuku ya kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa
kuwa kampuni zetu zinafanya biashara hivyo haikuwa rahisi kwa kampuni za simu
za mkononi kuwekeza bali UCSAF imetuwezesha kusambaza mawasiliano vijijini.
Vile vile ameiomba Serikali kuwasaidia kufikisha umeme kwenye minara kupitia Wakala
wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) kwa kuwa inawapa changamoto ya kuongeza
gharama za kuendesha minara hiyo na umeme wa jua hautoshelezi.
Ameongeza kuwa sisi
kama kampuni ya Halotel tunapata ushirikiano mkubwa kutoka ofisi za Wakuu wa
Mikoa na wilaya kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga minara bali
changamoto ipo kwenye ngazi za Halmashauri za upatikanaji wa ardhi na utatuzi
wa migogoro ya ardhi na ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mamlaka
husika ili kufanikisha ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano
vijijini.
Mwenyekiti Prof.
Sigalla amesema kuwa nguzo za uchumi mojawapo ni miundombinu kwa maana ya
barabara, bandari, reli na mawasiliano na ndiyo maana serikali imepeleka fedha
nyingi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18. Ametoa rai kwa wananchi kuwa
watoe ulinzi kwenye minara yote ya mawasiliano nchini kwa kuwa Serikali
inatumia kodi za wananchi kujenga minara. Ameongeza kuwa wananchi watumie fursa
ya mawasiliano kwa maendeleo na kujenga uchumi wao na maendeleo ya taifa. Pia ameyaomba
makampuni ya simu yote nchini ambayo yamepatiwa ardhi na serikali ya kijiji na kujenga
minara irudishe faida kwa wananchi wa eneo husika kwa kuwapatia fedha au huduma
za kijamii.
Amesisitiza kuwa
kampuni za mawasiliano zitumie fedha waliyopewa na Serikali kujenga minara na
kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwa wakati kwa kuwa ucheleweshaji wa
kutekeleza jukumu hilo unawanyima wananchi haki ya kupata huduma za
mawasiliano. Pia ameongeza kuwa kwa namna yoyte ile kampuni haziwezi kulipa
gharama za ucheleweshaji wa kujenga minara hiyo na upatikanaji wa huduma za
mawasiliano kwa wananchi na Serikali kwa
ujumla. “Maendeleo ni vita, ukipewa ruzuku na Serikali ya kujenga minara na
ukichelewesha ni hasara; hakikisheni mnakimbizana kukamilisha jukumu hilo kwa
wakati,” amesema Prof. Norman Sigalla King.
Aidha, ametoa rai kwa
kampuni za simu zinazopatiwa ardhi bure na Serikali za vijiji mbalimbali nchini
kote kutoa fedha kwa vijiji hivyo sehemu ya fedha wanazopata ili vijiji viweze
kunufaika na uwepo wa minara hiyo kwa kuwa kampuni zinafanya biashara. Ametanabaisha kuwa minara haina madhara kwa
wananchi ukilinganisha na usikilizaji wa simu za mkononi kwa muda mrefu zaidi
ya dakika tisa.
Amewatahadhirisha wananchi kuwa wananchi wasikilize simu kwa
muda mfupi na isizidi dakika tisa. “wananchi watumie vifaa vya kusikiliza simu
masikioni kwa wale ambao wanasikiliza simu kwa muda mrefu na minara inayowekwa
na UCSAF ni salama na tumieni simu kwa maendeleo chanya,” amesema Prof. Norman
Sigalla King. Pia ameipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya ya kujenga na
kusimamia miundombinu iliyopo kwenye sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano




0 Comments