Mwenyekiti wa Bodi ya
Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule, akisisitiza jambo wakati
akitoa taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko
huo katika halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya ujenzi wa barabara kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani), mjini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa
Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB), wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya
Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule hayupo pichani), wakati akitoa
taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo
katika halmashauri mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/16, mjini Dodoma
leo.
Meneja wa Mfuko wa
Barabara nchini (RFB), Bw, Eliud Nyauhenga akisisitiza jambo mara baada taarifa
ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo katika
halmashauri mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2015/16 kuwasilisha na
Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo Bw. Joseph Haule , mjini Dodoma leo.
...........
Halmashauri zote nchini
zilizobainika kutumia fedha za miradi ya ujenzi wa barabara kinyume cha
utaratibu kwa kubadili matumizi na kulipa miradi hewa zimetakiwa kuzirudisha
fedha hizo katika Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ili
zikafanye kazi iliyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya
Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule, amesema hayo wakati akitoa
taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa fedha zilizopelekwa na mfuko huo
katika halmashauri mbalimbali nchini kwaajili ya ujenzi wa barabara na kutumika
kwa kazi nyingine.
“Haikubaliki yaani
zaidi ya shilingi millioni 400, zitumike kinyume cha utaratibu kwa kununua
madawati, kompyuta, vifaa vya ofisi, kujenga maabara za shule za sekondari na
matumizi hewa kinyume na utaratibu wa matumizi ya fedha za mfuko wa barabara”,
amesema Bw, Haule.
Mwenyekiti huyo wa RFB
amezitaja halmashauri zinazohusika na matumizi mabaya ya fedha za barabara kuwa
ni Jiji la Tanga, Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Moshi, Songea, Kilolo, Nanyumbu, Masasi
na Ushetu.
Nyingine ni
halmashauri ya wilaya ya Kyerwa, Karagwe, Ngorongoro, Meru, Kondoa,
Kakonko, Kalambo, na Gairo.
Bw, Haule amesisitiza
kuwa hatua za kinidhamu na kijinai kwa wote watakaobainika kuhusika na matumizi
mabaya ya fedha za mfuko wa barabara zichukuliwe mara moja.
Naye meneja wa mfuko
wa barabara Bw, Eliud Nyauhenga amesema wamejipanga kuhakikisha fedha za
barabara zinatumika kama ilivyokusudiwa na bodi imeongeza wataalam wa ukaguzi
wa miradi inayotumia fedha za mfuko huo hivyo kuzitaka halmashauri kuongeza
umakini katika utekelezaji wa miradi ya barabara.
“Nasisitiza umuhimu wa
halmashauri zote kushirikiana na maabara za Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS),
zilizoko mikoani ili kuwezesha kazi za ujenzi wa barabara zinazofanyika kuwa na
ubora na viwango” amesema Bw, Nyauhenga.
Bodi ya Mfuko wa
barabara ambayo hutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika halmashauri
nchini imewataka wahandishi wanaosimamia fedha hizo kuongeza ufanisi ili
kuwezesha fedha hizo kutekeleza miradi mingi kwa wakati na kwa kuzingatia
thamani ya fedha.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano



0 Comments