Kaimu Mkurugenzi wa Maadili toka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Lambert Chialo (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akieleza umuhimu wa watumishi wa Umma kuzingatia maadili kazini, kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Bi. Mary Mwakapenda.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
....
....
Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali kupitia
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewaonya
watumishi wa Umma kutoa taarifa za serikali za siri na za kawaida kwa watu
ambao sio walengwa wa taarifa hizo.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Maadili
kutoka Wizara hiyo Lambert Chialo alisema kwamba kwa mujibu wa sheria ya
Usalama wa Taifa Na. 3 ya mwaka 1970 na marekebisho yake, Ibara ya 5(a) na (b),
adhabu ya uvujaji wa siri ni kifungo kisichozidi miaka 20.
“Hivi karibuni
tumeshuhudia taarifa za serikali za siri zikitumwa katika vyombo vya habari
pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii kitu ambacho ni kosa kisheria na ni kinyume
cha Kanuni za Maadili ambapo inasisitizwa kuwa na matumizi sahihi ya taarifa”,
alisema Chialo.
Chialo aliongeza
kwamba lengo la serikali si kuficha taarifa kwa wadau wake, bali taarifa
zinazotolewa zinapaswa kutolewa kwa utaratibu maalumu na kupelekwa kwa watu
wanaopaswa kupokea taarifa hizo (walengwa). Aidha, taarifa zinazotolewa na
taasisi husika lazima zipate idhini kwa Uongozi husika kabla ya kupelekwa kwa
wadau.
Akiongelea suala la
matumizi mabaya ya Ofisi, Chialo alisema kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa
wakitumia nafasi walizonazo kwa manufaa
yao binafsi na sio ya Umma, kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na watumishi
watakaogundulika watawajibishwa kwa mujibu wa Kanuni na taratibu.
Watumishi wa Umma
wanapaswa kufahamu kwamba serikali inaendelea kufatilia matendo yote yasiyo ya
kimaadili na kuchukua hatua kila inapobidi. Aidha, wananchi wanaombwa kutoa
ushirikiano kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili katika taasisi za umma
kila wanaposhuhudia matukio hayo.
“Tunalo dawati la
msaada kwa ajili ya kupokea maoni, malalamiko, ushauri na taarifa mbalimbali
katika kuhakikisha utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi unaboreshwa”
alisema Chialo.
Chialo alitoa rai kwa
wananchi wote kwa ujumla, kuzingatia swala la maadili kuanzia ngazi ya familia.
Aidha, inasisitizwa viongozi na wasimamizi wa kazi kuendelea kuelimisha
watumishi kuhusu suala la maadili na kuhakikisha watumishi wanaishi kwa
kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa vitendo.

0 Comments