Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba
....
Jovina Bujulu-MAELEZO
Sekta ya kilimo nchini
ni kitovu cha maendeleo ya viwanda kwa kutoa masoko na malighafi za viwandani
ambapo inaajiri Watanzania wengi takribani zaidi ya asilimia 67.
Katika utekelezaji wa
Mpango wa Pili wa Maendeleo, Serikali inaendelea kuimarisha mafanikio
yaliyofikiwa katika sekta ya kilimo ikiwemo kuimarisha masoko ya kilimo ili
sekta hiyo iendelee kuwa na tija kwa wakulimananchi na taifa kwa ujumla.
Hivi karibuni
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilitangaza kufuta ada na
tozo mbalimbali katika baadhi ya mazao ya biashara ili kumpa unafuu mkulima
wakati wa kuuza mazao yake.
Hatua hiyo ni mwanzo
mzuri wa kuimarisha sekta hiyo hasa wakati huu ambapo Serikali ya Awamu ya Tano
imetangaza nia yake ya kuimarisha uchumi wa kati na viwanda.
Serikali iliamua
kufuta na kupunguza ada na tozo imedhamiria kumaliza kero na kilio cha muda
mrefu cha wakulima ambao wamekuwa wakilalamikia tozo hizo kwa madai kuwa
zinawanyonya.
Aidha, uamuzi huo
unategemea kuwapunguzia mzigo mkubwa wa malipo ambao umekuwa ukiwaelemea
wakulima hao, hivyo kuwapa unafuu mkubwa na kuwapatia faida.
Akiwasilisha hotuba
ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alizitaja baadhi ya tozo zilizofutwa katika zao
la tumbaku kuwa ni mchango wa ushirika wa mkoa, mchango kwa ajili ya gharama za
masoko ya ushirika na chama cha msingi cha ushirika, dhamana ya benki kuu ya
Tanzania na fomu ya maombi ya leseni za tumbaku.
Ada na tozo nyingine zilizotajwa
kuwa ni kodi ya leseni ya kununua tumbaku kavu na mbichi kiwandani, leseni ya
kuuza tumbaku nje ya nchi na tozo ya Baraza la Tumbaku.
Pamoja na kufuta tozo
na ada katika baadhi ya mazao, Serikali pia imetoa punguzo katika zao la
tumbaku ambapo kodi ya leseni ya tumbaku kavu itakuwa dola za kimarekani 2,000
badala ya dola 4,000.
Aidha, leseni ya
kusindika tumbaku imepungua kutoka dola za kimarekani 10,000 hadi 5,000 ambapo Serikali
imechukua hatua hizo ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo wakiwemo wakulima
wadogo.
Kupitia bodi ya
mazao, Serikali itaendelea kuimarisha soko la mazao ya asili hasa mazao ya
jamii ya mikunde ili kukidhi mahitaji ya zao hilo katika soko la India na zao
la muhogo kwa ajili ya soko la China.
Tozo na ada nyingine
zimepunguzwa katika zao la kahawa, ambapo ada ya leseni ya ghala la kahawa, leseni ya kukoboa kahawa,
kuuza nje ya nchi kahawa iliyosindikwa na leseni ya kununua kahawa kwa kampuni
na vyama vya ushirika zimefutwa.
Tozo nyingine
zilizopunguzwa kwenye zao la kahawa ni ya fomu ya kuomba leseni ya kuuza kahawa
ya kijani, leseni ya ghala na leseni ya kukoboa na kusindika kahawa pia
zimefutwa.
Kwa upande wa zao la
sukari jumla ya ada 17 zimefutwa ambazo baadhi ni ada hizo ni ya leseni ya
uingizaji sukari ya viwandani, ada ya leseni kamili ya uzalishaji sukari mkubwa
na mdogo, leseni ya muda ya uzalishaji sukari uwekezaji mdogo, leseni ya
marudio kila baada ya miaka mitatu na ada ya leseni ya kuchakata miwa.
Vilevile ada ya
kusajili kwa waagizaji wakubwa na wa
kati, na ya wafanyabiashara wa sukari ya matumizi ya kawaida ikiwa ni pamoja na
ada ya kupata kibali cha kuingiza sukari ya viwandani zimefutwa pia.
Mazao ya pamba, chai
na korosho pia yamo katika kufutiwa tozo na ada. Hii ni pamoja na tozo ya kituo
cha kununulia pamba katika ngazi ya Halmashauri na tozo ya maendeleo ya elimu
katika Halmashauri ya Meatu.
Katika zao la chai,
tozo kwa ajili ya gharama ya uendeshaji wa vyama vya wakulima na ada ya leseni
ya kununua korosho zimefutwa, ambapo wakulima na wafanyabiashara watapata
unafuu wakati wa kuuza mazao yao.
Katika kuhakikisha wakulima
wanaendelea kunufaika na kilimo, Serikali pia imefuta baadhi ya ada katika
pembejeo ya mbolea ambapo wafanyabiashara wa mbolea hawatalipia usajili wa
mbolea, ada ya leseni na usajili wa mzalishaji.
Akizungumzia kufutwa
kwa tozo na ada hizo, wakati wa maonesho ya kilimo (Nanenane) yaliyofanyika Kitaifa
hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, Naibu Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate Ole Nasha alisema kuwa Serikali ilifikia
hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa tozo hizo hazikulenga
kuwakwamua wakulima katika wimbi la umaskini badala yake ziliwazidishia
umaskini.
Aliendelea kusema
kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliamua kufuta tozo na ada hizo ili kutimiza
azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote
vilivyokuwa vikiwakabili wakulima ili kuwainua na kukuza uchumi.
Aidha, Serikali za
Mitaa zimeagiza kuacha kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa kutoka
Halmashauri moja kwenda nyingine ili kurahisisha na kuwapunguzia wakulima mzigo wa kulipa kodi.
Kutokana na kupunguza
kodi, tozo na ada mbalimbali katika
mazao hayo ya biashara wakulima wanatakiwa kuitumia nafasi hiyo kwa manufaa yao
kwa kujiongezea faida ikiwa ni pamoja na kuzingatia kilimo bora chenye tija kwa
ajili ya kujipatia mazao bora yanaweza kukabiliana na soko la ushindani ndani
na nje ya nchi hatua itakayowasaidia kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
0 Comments