Mwenyekiti wa Kanisa la Good News For All Ministry
Askofu Dkt. Charles Gadi (wa pili toka kulia) pamoja na wachungaji wa kanisa
hilo wakifanya maombi maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo jijini Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa Kanisa la Good News For All Ministry
Askofu Dkt. Charles Gadi (katikati) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari
(hawapo pichani) wakati akifanya maombi maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo
jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu wa kanisa hilo Mchungaji Palemo Massawe
na kushoto ni Mchungaji wa kanisa hiliAndrew Thomas.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kanisa la
Good News For All Ministry Askofu Dkt. Charles Gadi wakati akifanya maombi
maalumu ya kuombe mvua mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Askofu wa kanisa la
Good News For All, Dkt. Charles Gadi ametoa wito kwa wananchi na serikali
kuyatunza mazingira na uoto wa asili ili kuchangia uwepo wa hali nzuri ya hewa.
Hayo yameelezwa leo
Jijini Dar es Salaam na Askofu Gadi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari ambapo aliongoza maombi maalum kwa lengo la kuombea tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Utabiri
wa Hali ya Hewa juu ya uwezekano wa
kutokea kwa upungufu mkubwa wa mvua za vuli katika mikoa mingi hapa nchini.
Askofu Gadi amesema
kuwa wananchi wote wanapaswa kulinda mazingira ikiwemo kupiga vita ukataji ovyo wa miti na badala
yake wapande miti kwa bidii ili kuilinda mazingira kutokana na uharibifu
unaosababisha ukame unaotokana na ukosefu wa mvua.
Aidha askofu huyo amesema kuwa wao kama
viongozi wa dini wanakubaliana na utabiri wa kisayansi uliotolewa ambao mara
nyingi umekuwa ukifanikiwa, lakini haitokuwa sawa kusubiri hadi hali hiyo ya
ukame itakapotokea wakati Mungu amewapa Imani na mamlaka ya kuomba dhidi ya
majanga kama hayo.
“Good News for All kwa
kushirikiana na madhehebu mbalimbali tumekuwa tukiendesha mikutano ya kuiombea
nchi dhidi ya ukame tangu mwaka 2006 ambapo ni zaidi ya miaka 11 sasa tunamshukuru
na Mungu amekuwa akijibu maombi yetu,” alisema Askofu Gadi.
Pia, Askofu Gadi
amesema kuwa kutokana na uzoefu walionao wanatoa wito kwa viongozi wengine wa
dini kufanya maombi ili ukame huo usitokee.
“Ukame ni jambo baya
kwa uchumi, ni baya kwa afya ya watu na baya kwa viumbe hai wote wakiwemo
wanyama na mimea hivyo tuungane kwa pamoja katika kuliombea jambo hili,”
alifafanua Askofu Gadi.
Aidha, Askofu gadi
amesema “jambo la kufurahisha ni kwamba mvua ni hazina nzuri ya Mungu, tena
ndicho kitu cha thamani ambacho alikiacha duniani kwaajili ya kuendesha uhai
aliouumba hususani kwa viumbe hai.
Vilevile Askofu Gadi
amefafanua kuwa maandiko matakatifu katika Biblia yanaonyesha kuwa mvua ni mali
ya Mungu na ameahidi pasipo shaka kwamba tukimwomba atatupatia, ndiyo maana wana
Imani na ujasiri kuomba dhidi ya ukame na majanga mengine kila mara na Mungu
amekuwa mwaminifu kwa neno lake kwa kujibu maombi.
“Katika kitabu cha Matendo
ya mitume 14:17, lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema
akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno akiwashibisha mioyo yenu
chakula na furaha,” alieleza Askofu Gadi.



0 Comments