Jonas Kamaleki-MAELEZO
Muda mfupi baada ya kula kiapo,
Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, ametoa onya
kali kwa majingili nchini na kuwataka kuacha mara moja vitendo hivyo.
Dkt. Kigwangalla ametoa onyo hilo leo Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuapishwa mawaziri na naibu mawaziri.
“Majangili waanze kukimbia wenyewe
pale wanapowaona wanyama kwani tutawashughulikia ipasavyo na
kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi viovu katika nchi yetu,” alisema
Dkt. Kigwangalla.
Kuhusu utalii, Dkt. Kigwangalla
amesema kuwa watalii wamekuwa wakiongezeka lakini si kwa kiwango cha
kuridhisha hivyo Serikali itafanya juhudi za makusudi kutangaza vivutio
vya utalii kwa njia za kisasa ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa ubunifu katika
kujitangaza itabidi utumike ili kuhakikisha Tanzania inavutia watalii
wengi kutoka nje hususan soko jipya la China na nchi nyingine ikiwemo
Marekani na nchi za Ulaya.
Kwa kufanya hivyo pato la Taifa kutokana na utalii litaongezeka kuliko ilivyo sasa, alisema Kigwangalla.
Aidha, Waziri huyo wa Maliasili na
Utalii amesema atashirikiana na wizara nyingine kukomesha migogoro ya
wakulima na wafugaji ili lipatikane suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman
Jafo, amesema atahakikisha watumishi wa umma katika wizara yake
wanafanya kazi kwa kujituma zaidi na kuachana na kufanya kazi kwa
mazoea.
Kwa mujibu wa Jafo, uadilifu,
uwajibika na nidhamu ni mambo ambayo yatatiliwa mkazo katika wizara yake
ili kuwa na utumishi wenye tija.
Amewataka wakuu wa mikoa, wilaya
kufanya kazi kwa mashindano ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo
katika sehemu husika na kuchochea ukuaji wa uchumi hasa wa viwanda.
“Wakuu wa mikoa na Wakurugenzi wa
Halmashauri muwe vinara katika utendaji wenu mkiwasimamia walioko chini
yenu kwa weledi ili muweze kwenda na spidi ya Serikali ya Awamu ya
Tano,” alisema Jafo.
Naye Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza akizungumza baada ya
kuapishwa amesema atahakikisha sekta ya habari inapewa kipaumbele kwani
habari ni jambo muhimu katika suala zima la mawasiliano.
Mhe. Shinza atahakikisha weledi
katika sekata ya habari unazidi kuimarishwa ilikuondoa upotoshwaji ambao
umekuwa ukijitokeza katika baadhi ya vyombo habari.
Kuhusu upatikanaji wa habari kwa
sehemu kubwa ya watanzania, Shonza amesema atajitahidi kufanya habari
ziwafakie watanzania wengi Zaidi ili kujenga jamii yenye ufahamu wa
masuala mbalimbali yanayoihusu nchi yao.
Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha jumla ya
Mawaziri nane na Manaibu Mawaziri 16 ambao wameanza kazi mara baada ya
kuapishwa kwa kuhudhuria kikao cha Maalum cha Baraza la Mawaziri.
Baadhi ya mawaziri waliokula kiapo
leo ni Mhe. Angella Kairuki (Madini), Mhe. George Mkuchika (Ofisi ya
Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe. Hamis
Kigwangwalla (Maliasili na Utalii) na Suleiman Jafo (Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).
Kwa upande wa Manaibu Mawaziri,
Mhe. Rais amewaapisha jumla 16 ambao baadhi yao ni Mhe. Stella Manyanya
(Naibu waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Mhe. William Ole Nasha
(Elimu, Sayansi na Teknolojia), Dkt. Faustine Ndungulile (Afya, Maendelo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Mhe. Stella Ikupa (Ofisi ya Waziri
Mkuu, Watu wenye Ulemeva) na Mhe. Juliana Shonza (Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo)

0 Comments