Random Posts

Halmashauri ya mji wa Kibaha yatenga hekari 2,000 kwa ajili ya wanawake na vijana

 Mkuu Wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama ,Mwenye Nguo nyeupe akitembelea bidhaa mbalimbali za wajasiriamali kabla ya shughuli ya kukabidhi hundi kwa vikundi mbalimbali vilivyogawiwa fedha za mfuko Wa wanawake na vijana katika halmashauri ya mji Wa Kibaha Mkoani Pwani .(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani,imeandaa ardhi ya hekari 2,000 kwa ajili ya kilimo kwa wanawake na vijana katika eneo la Misugusugu,ili kujikomboa na umaskini.

Kati ya hekari hizo hekari 1,000 ni kwa ajili ya wanawake na nyingine 1,000 ni kwa ajili ya kundi la vijana ambapo maeneo hayo ni bure na sio mali yao milele lengo ni kuyaendeleza .

Aidha halmashauri hiyo imetenga kiasi cha sh.milioni 100 kwenye kipindi cha July –Septemba  mwaka huu ambazo ni asilimia 10 ya mfuko wa vijana na wanawake.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama aliyasema hayo wakati akizindua kampeni ya viwanda vyetu ,wilaya yetu ,””uzinduzi ambao ulioambatana na makabidhiano ya hundi za mikopo kwa vikundi mbalimbali vilivyopo halmashauri ya mji huo.

Hata hivyo ,wameandaa eneo lenye hekari si chini ya 50 kwa ajili ya viwanda kwa  wanawake na vijana lenye ukubwa huo.

Assumpter alisema mpango huo unalenga kutoa ajira kwa wananchi wakiwemo vijana na wanawake na kuzalisha uzalishaji wenye tija na kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa zinazozalishwa .

Aliwataka wajasiriamali wilayani humo,kuzalisha bidhaa bora,safi zilizo kwenye vifungashio ili kupata soko kirahisi.

Alisema  wakati nchi ikienda kwenye kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji ni lazima wabadilike kwa kuanza kuboresha bidhaa zao sio ili mradi ,kwa lengo la kuongeza thamani .

“Tengenezeni bidhaa zenye viwango,hii itawasaidia mtafutwe badala ya kutafuta wateja,biashara ni matangazo na kizuri chajiuza”alifafanua Assumpter.

Akizungumzia fedha za mkopo ,Assumpter alitoa rai fedha zinazotolewa kwa makundi hayo ,zirejeshwe kwa wakati na zitumike kwa makusudi yaliyoombewa.

Alisema awamu ya tano sio ya kula fedha na fedha yake hailiwi bila ya utaratibu uliowekwa hivyo fedha hizo inapaswa kutumika vizuri na kurejeshwa kwa wakati.

Nae afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Mji wa Kibaha,Leah Lwanji alisema,katika awamu ya kwanza mwaka wa fedha 2017-2018 halmashauri imetenga milioni.100 itakayonufaisha vikundi 50 kwa wanachama 320.

Alielezea ,halmashauri hiyo imekuwa ikitenga fedha mwaka hadi mwaka na kuleta manufaa kwa makundi hayo ambapo mwaka 2010 walianza kukopesha mil.12 na kufikia mwaka 2016 ilikopesha mil.174 .

Alisema idara ya maendeleo ya jamii imefanya mazungumzo na SIDO  ili kuona namna nzuri ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati ikiwa ni sanjali na kuwezesha uandaaji wa michoro viwanda vidogo,uwezeshaji wa mafunzo na upatikanaji wa mashine mbalimbali.

Leah aliwahamasisha vijana wanaomaliza mafunzo ya VETA Pwani -kupitia program maalum ya YEE kujiunga kwenye vikundi ili kutumia fursa za uwezeshaji hatimae kujipatia mitaji.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,Jennifer Omolo,alisema mwaka jana halmashauri ilitoa mkopo wa sh.mil.174 ,kwa mwaka 2017 wameshakusanya bilioni moja ambayo wametenga asilimia 10 sawa na mil.100 ambayo itakwenda kwa wanawake na vijana.

Alibainisha vikundi hivyo ni 50 na kila kata moja kati ya 14 zilizopo kwenye halmashauri hiyo ina vikundi vitatu ambavyo vitapatiwa milioni.nne  kila kikundi.

Jennifer alifafanua,kufuatia kampeni iliyozinduliwa,halmashauri inashirikiana na SIDO kuhakikisha wanawake wanaingizwa kwenye vikundi vya watu 20 kila kimoja  ili kuweka viwanda vidogo vidogo.

Mkurugenzi huyo alisema wanawake wanakosa soko lakini kutokana na mkakati huo itawasaidia kuzalisha wenyewe badala ya kununua viwanda vingine .

“Tunashirikiana na Nyumbu JKT ambao wanatengeneza vifaa kwahiyo watapata vifaa kwa bei nafuu kwa ajili ya viwanda hivyo”alisema Jennifer.

Post a Comment

0 Comments