Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Serikali imesema kuondolewa kwa
kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vya ujenzi kwa lengo la
kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi kutawanufaisha
wafanyabiashara wachache kuliko wananchi wa kawaida na kupunguza mapato
ya Serikali.
Hayo yamesemwa Bungeni leo Mjini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb),
wakati akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Godbless Lema juu
ya Serikali kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi.
“Matumizi ya vifaa vya ujenzi ni
mtambuka, ni vigumu kutambua kama mnunuzi atatumia kwa ujenzi wa makazi
binafsi, biashara au miundombinu kama barabara” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza kuwa
lengo la kutoza kodi ni kuiwezesha Serikali kuwa na mapato ya kutosha
ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma
muhimu za kijamii kwa Wananchi wake.
“Uhai wa Taifa lolote ni kodi
hakuna maendeleo yanayopatikana katika Taifa lolote bila kodi hivyo
makusanyo ya kodi ndio yanasababisha Serikali kuweza kutoa huduma nyingi
bure kwa wananchi wake”. Amefafanua Dkt. Kijaji.
Hata hivyo Dkt. Kijaji amesema
kuwa nyumba zinazojengwa na kuuzwa na Shirika la Nyumba la Taifa ni
mradi wa kibiashara na si huduma, pia wauzaji wa nyumba hapa nchini ni
wengi hivyo kuondoa kodi ya VAT kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la
Nyumba la Taifa peke yake utakua ni ubaguzi kwa wauzaji wengine wa
nyumba ikiwa na kuikosesha Serikali mapato kwa manufaa ya Taifa

0 Comments