Ndugu Wananchi,
Siku
ya Kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 14 ya Mwezi
Novemba.
Siku hii ilianzishwa mwaka 1991 na mashirika mawili ya kimataifa (Shirika
la Ugonjwa wa Kisukari Duniani na Shirika la Afya Duniani) baada ya kuona ugonjwa
wa kisukari unaongezeka sana duniani kote.
Tanzania
kama zilivyo nchi nyingine zote Duniani inaadhimisha siku hii, ambapo Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na Chama cha
Ugonjwa wa Kisukari Tanzania, kwa kutoa
elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na
ugonjwa wa kisukari.
Ndugu Wananchi,
Ugonjwa
wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi
kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata
nishati lishe.
Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji
kichocheo cha insulin.
Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai
ili kutengeneza nishati lishe.
Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo
hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha sukari
kinabaki kikubwa kwenye damu.
Kwa bahati mbaya, watu wengi hawajitambui ya kuwa wana ugonjwa huu.
Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema.
Dalili za kisukari
ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua
uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na mojawapo kati
ya dalili hizi nenda hospitali ukapime sukari.
Ndugu Wananchi,
Asilimia
80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea,
ikiwemo Tanzania.
Tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007
kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani, mwaka 2013
kulikuwa na wagonjwa 382 milioni duniani kote.
Ifikapo mwaka 2035 inatarajiwa kuwa
na wagonjwa 592 milioni. Katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari
19.8 millioni mwaka 2013 ambapo nusu ya wagonjwa hawa walikuwa
hawajaanza matibabu.
Wagonjwa hao wataongezeka kufikia million 41.1 ifikapo
mwaka 2035. Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini
Tanzania ulionyesha ya kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25
na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
Katika
nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya 8.
Kwa upande wa watoto, hadi kufikia
mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watoto elfu mbili wameingizwa kwenye reiista
za watoto kwenye kliniki za ugonjwa wa kisukari, ikiwa ni baadhi tu ya watoto
wote wenye ugonjwa huu hapa nchini.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya
Kisukari Duniani mwaka 2017 ni “Wanawake
na kisukari; haki yetu ya afya bora ya baadae”. Kwa lugha ya kigeni ni ‘ Women and Diabetes ; Our right to a
healthy future’.
Kauli mbiu hii imetolewa na shirika la Afya Duniani,
itumike ulimwenguni kote, kuhamasisha huduma za kisukari kwa wanawake kwa ajili
ya afya bora ya sasa na baadae.
Mambo
yanayoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari ni pamoja na ulaji usiofaa
hasa matumizi ya mafuta na sukari kwa wingi, uzito uliozidi, kutofanya mazoezi na
unywaji pombe kupita kiasi.
Aidha
mambo mengine yanayo ongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza
ni pamoja na matumizi ya chumvi kwa wingi pamoja na uvutaji wa sigara na bidhaa
za tumbaku.
Ndugu Wananchi,
Ili
kuzuia ugonjwa wa kisukari ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji
bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa
kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari
hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.
Madhara au athari za ugonjwa
wa kisukari ni upofu, shinikizo la damu kuwa juu, kiharusi, ugonjwa wa figo,
kupungua nguvu za kiume, upungufu wa kinga mwilini, kuwa na vidonda hasa
miguuni visivyopona mapema pamoja na ganzi katika miguu au mikono na mwisho kukatwa
mguu kwa sababu ya kuathirika mishipa ya damu na mishipa ya fahamu miguuni.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo
kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa.
Serikali pia inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa
kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo
kisukari.
Serikali imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na za
binafsi katika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Kwa
kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993, serikali
ilitoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu na
inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani wetu kuhakikisha kuwa
dawa muhimu zinapatikana.
Kwa sasa watoto wote na vijana chini ya miaka
ishirini na saba walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote bila malipo kupitia
kliniki za kisukari zilizopo nchini.
Kwa sasa dawa za mstari wa kwanza na
mstari wa pili za matibabu ya kisukari zipo kwenye mwongozo wa matibabu wa
Kitaifa na zinapatikana kupitia bohari kuu ya dawa.
Kuanzia
mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango wa kudhibiti
ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki hizo hadi katika ngazi ya
vituo vya afya pamoja na kuwapatia wananchi elimu ya ugonjwa wa kisukari ili
waweze kushiriki kikamilifu kwenye kinga na tiba ya magonjwa haya.
Tanzania
inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la
mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe wa kudhibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine kuhakikisha ya
kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanapungua kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ilizundua mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambao ulishirikisha wadau mbalimbali.
Ndugu
wananchi,
Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda
mrefu bila kuwa na dalili zilizotajwa hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari
inavyokuwa juu, inaharibu mishipa ya damu na ya fahamu, macho na kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa kufanya kazi, na miguu
kufa ganzi na kuwa vidonda, au kunyauka kwa kukosa mzunguko wa damu.
Hivyo ninatoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima
afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema. Ni vyema
kila mwenye umri wa miaka arobaini na kuendelea akapima afya yake angalau mara
moja kwa mwaka ili kutambua hali yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una
ugonjwa wa kisukari tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na
wataalam wa afya.
Kama sehemu ya maadhimisho haya, Wizara kwa kushirikiana
na Chama cha Kisukari Tanzania tutafanya zoezi la uchunguzi kwenye shule za
sekondari za Kisutu na Jangwani. Pia Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa kupitia
Waratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ngazi ya Mikoa na Wilaya watafanya
mazoezi na pia uchunguzi.
Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa
na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa
watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana
na ugonjwa ya kisukari.
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA

0 Comments