Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa
sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake
mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya
kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya
kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa
kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej.
Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki (kulia).
Na Hamza Temba, Dodoma
.............................. .............................. ...
Serikali
imesikia kilio cha wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii nchini na
kuamua kuongeza muda wa miaka miwili ya umiliki wa leseni za vitalu 95
vya uwindaji wa kitalii ambazo zilikuwa ziishe muda wake tarehe 31
Desemba mwaka huu (2017).
Uamuzi
huo umefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla
wakati wa kikao cha majumuisho na watendaji wa Wizara hiyo muda mfupi
baada ya kumalizika kwa mkuano wa wadau wa sekta hiyo ulioandaliwa na
Wizara hiyo mjini Dodoma jana.
Akizungumzia
uamuzi huo Dk. Kigwangalla alisema, lengo ni kuwapa muda wawekezaji hao
ili waweze kujiandaa na mabadiliko ya mfumo mpya wa utowaji wa leseni
za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ikiwemo kurudisha
baadhi ya gharama za uwekezaji walizoweka katika vitalu hivyo.
Awali
akizungumza katika mkutano huo wa wadau Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini, Michael Mantheakis
alimuomba Waziri Kigwangalla kuwaongezea muda wa umiliki wa leseni zao
kuanzia miaka mitano au mitatu na nusu ili waweze kurudisha gharama za
uwekezaji walizowekeza katika vitalu hivyo ikiwemo ujenzi wa
miundombinu, makambi na vifaa vyake pamoja na maji.
Hata
hivyo, Waziri Kigwangalla aliweka wazi msimamo wa Serikali wa kutimiza
azma yake ya kuingia kwenye utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu
vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na kusema kuwa kamwe
haitorudi nyuma na kwamba utekelezaji wa zoezi hilo hauwezi kusubiri
muda mrefu kiasi hicho.
Akizungumzia
kuhusu hatua ya utekelezaji wa utaratibu huo, Waziri Kigwangalla
alisema kwa sasa taratibu za kuandaa Sheria za usimamizi zinaendelea na
zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2018 pamoja na kanuni zake
zinazotarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2018.
Aidha,
alisema mfumo maalumu wa kielektroniki unaandaliwa ambapo maombi yote
ya leseni za umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada
yatafanyika kwa uwazi kwa njia ya mtandao.
Alisema
baada ya kukamilika kwa taratibu zote na mfumo huo mpya wa utoaji wa
leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na maombi
kuwasilishwa, mnada wa kwanza utaanza tarehe 1 Julai, 2018 kwa kuanza
kunadi vitalu 61 ambavyo kwa sasa havina wawekezaji.
Mnada
wa pili utafanyika mwaka 2020 baada ya kuisha kwa muda huo wa nyongeza
wa miaka miwili ukihusisha vitalu 95 vilivyoongezewa muda wa umiliki wa
leseni pamoja na vitalu vingine endapo vitabaki katika mnada huo wa
kwanza kwa sababu mbalimbali.
Alisema
sheria na kanuni zinazoandaliwa hivi sasa zitazingatia mambo muhimu
ikiwemo kuwapa nafasi watanzania wenye mitaji midogo kuweza kuingia
kwenye biashara hiyo pamoja na kuweka adhabu kali dhidi ya
wafanyabiashara watakaohujumu biashara hiyo kwa makusudi.
Mkutano
huo wa siku moja ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja
Jenerali Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki,
wakurugenzi, wakuu wa vitengo na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya
wizara hiyo na waandhishi wa habari.
Oktoba 22 mwaka huu (2017) wakati akiongoza kikao cha wadau wa sekta ya Maliasili na Utalii mjini
Dodoma, Waziri Kigwangalla alitangaza kufuta leseni za vitalu vya
uwindaji wa kitalii zilizokuwa zianze mwezi Januari, 2018 ili kupisha
utarartibu mpya wa utoaji wa leseni hizo kwa njia ya mnada ikiwa ni
mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta hiyo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa
sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake
mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya
kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya
kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa
kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce
Nzuki.
Katibu
Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi
(kushoto) akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Maliasili
na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mdau wa sekta ya uwindaji wa kitalii, Dk. Licky Abdallah akizungumza katika mkutano huo.
Mdau
wa sekta ya uwindaji wa kitalii ambaye pia ni mmilikia wa kampuni ya
uwindaji wa kitalii ya Bushman Hunting Safaris, Talal Abood akiwasilisha
mapendekezo yake katika mkutano huo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisikiliza kwa makini
mapendekezo ya wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano
uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
0 Comments