Kamishna wa Secretariati ya Maadili ya Viongozi
wa Umma Jaji Mstaafu Harold Nsekela akielezea jambo mbele ya Waandishi wa
Habari kuhusu tarehe ya mwisho ya kupokea Matamko ya Mali za Viongozi leo
Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu anayeshughulikia Maadili ya Viongozi wa Siasi Waziri Kipacha.
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Kamishna
wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold
Nsekela amewahimiza Viongozi wa Umma kukamilisha taratibu za ujazaji wa fomu za
tamko la rasilimali na madeni kabla ya Disemba 31 mwaka huu.
Ametoa
kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
Habari kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kiongozi wa umma
kupeleka tamko kwa maandishi lililo katika hati rasmi linaloorodhesha mali au
rasilimali za kiongozi na familia yake kwa Kamishna wa Maadili kila mwisho wa
mwaka.
Jaji
Mstaafu Nsekela amesema kuwa fomu za tamko hilo zinapatikana kwenye tovuti ya
Sekretarieti ya maadili ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz
hivyo ametoa wito kwa viongozi ambao hadi sasa hawajapata fomu kutumia tovuti
hiyo kupata fomu kwa urahisi.
“Kwa
kuzingatia kifungu cha 9 (1) (a) na (c) cha Sheria na Maadili ya Viongozi wa
Umma, viongozi wapya wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizi
ndani ya siku thelathini baada ya kupewa wadhifa fulani pia anapofika mwisho wa
kutumikia wadhifa huo anapaswa kujaza fomu na kuzirejesha katika ofisi yetu,”alisema
Jaji Mstaafu Nsekela.
Jaji
Mstaafu Nsekela amefafanua kuwa fomu hizo zinatakiwa kuwasilishwa katika Ofisi
ya Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma zilizopo Jijini Dar es Salaam au
katika ofisi zao za Kanda zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha,
Mtwara, Tabora, Pwani na Mbeya.
Kwa
upande wake Afisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti hiyo, Filotheus Manula amesema
kuwa kujaza fomu hizo ni takwa la kikatiba hivyo Viongozi wa Umma wahakikishe
wanajaza fomu hizo bila kudanganya.
“Ni
kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 15(c) cha Sheria za Maadili ya Viongozi wa Umma
kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko bila sababu ya msingi kwani sheria hizi
hazimzuii kiongozi kumiliki au kuwa na mali nyingi bali mali hizo zinatakiwa
kutolewa maelezo ya chanzo cha upatikanaji wake,” alisema Manula.
Aidha,
Manula amefafanua kuwa kosa hilo linaweza kumpelekea muhusika kuonywa au kupewa
adhabu ya kushushwa cheo, kusimamishwa, kufukuzwa kazi pamoja na kupelekwa
Mahakamani.
Vile
vile Manula amesema kuwa kwa sasa hali ya uadilifu kwa Viongozi wa Umma
inaridhisha kwani ukiukwaji wa maadili umepungua kwa kiasi kikubwa.

0 Comments