JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO
TAARIFA KWA UMMA
TAMKO MHESHIMIWA FAUSTIN NDUNGULILE (MB) NAIBU
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WATOTO
WANAOINGIA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2018
Napenda kutumia fursa hii kutoa ujumbe kwa
watoto wa Tanzania, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla katika kipindi hiki cha
ambacho watoto wetu wanajiandaa kujiunga na kidato cha Kwanza katika Shule za
Sekondari kwa mwaka wa masomo 2018. Aidha, nawapongeza watoto wote
waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kwa mwaka huu. Hii ni fursa
muhimu ya kupata haki ya msingi ya kuendelezwa na hivyo kuwajengea watoto
msingi madhubuti wa maisha ya baadaye kwa kutoa elimu na kuwa na jamii
iliuyobora.
Elimu kwa watoto ni moja ya njia bora za
kupunguza umasikini. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Benki ya Dunia, kila
mwaka wa elimu kwa mwanamke unaongeza thamani ya pato lake la baadaye kwa
asilimia 15 na asilimia 11 kwa mwanaume. Kadhalika, nafasi ya elimu kwa mtoto
wa kike na wa kiume husaidia katika makuzi bora kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili,
na kijamii. Hivyo, ni vyema wazazi, walezi na watoto wenyewe wafahamu kuwa
kuwaendeleza watoto wetu ni njia bora ya kutatua chjangamoto mbalimbali za
maisha kwa maendeleo ya jamii yetu.
Nawaasa watoto wote wa kike na wa kiume
kuzingatia wajibu wao na kutumia ipasavyo fursa hii muhimu ya kujiendeleza.
Nawataka watoto kujiepusha na vitendo viovu kama vile masuala ya ngono, vileo,
madawa ya kulevya na matumizi mabaya ya simu za mkononi kwani vinaweza
kuhatarisha afya, usalama na kuwapotosha kimaadili hivyo kuathiri haki yao ya
kuendelezwa na kuzima ndoto za maisha yao ya baadaye.
Watoto wote wa kiume na wa kike watambue kuwa
wao ni hazina ya pekee katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa letu. Aidha,
napenda watoto wafahamu kuwa fursa ya elimu ambayo wameipata ni maandaliziu ya
kuwawezesha kubeba dhamana ya kufikisha nchi yetu katika uchumi wa kati na wa
viwanda kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango wa
taifa wa maendeleo ya Miaka Mitano (2016/17- 2020/21) na Sera ya Maendeleo ya
Mtoto Tanzania (2008).
Kwa kuzingatia hayo, Serikali itahakikisha
watoto wote wanaendelezwa hadi kidato cha Nne ikiwa ni jitihada ambazo
zimeasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe
Magufuli. Kwa kutambua juhudi hizi za Serikali, iwe ni mwiko kwa mzazi
kutompeleka mtoto kujiunga na elimu ya Sekondari kwa kisingizio chochote kile.
Natumia fursa hii pia kuwakumbusha Watanzania
wote kuwa vitendo vya kufanya ngono, kuoa na kuwapa mimba wanafunzi
havikubaliki na hivyo wenye tabia hizo waache mara moja. Ikumbukwe kuwa kumpa
mimba mtoto au mwanafunzi ni kosa la kijinai na kwa yeyote atakayebainika
kufanya hivyo ikumbukwe adhabu yake ni kifungo cha miaka 30.
Aidha,
natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali
za mitaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika madawati ya jinsia na Watoto
yaliyopo katika vituo vya Polisi pale watakapobaini mzazi au mlezi amefanya hila
kuzuia Mtoto kupata haki yake ya kuendelezwa.
Ninawatakia
Mwaka mpya wenye furaha na mafanikio watoto, wazazi na watoto wote wanaoanza
masomo ya Sekondari kwa mwaka 2018 na pia wanaoendelea.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki Watoto wa Tanzania.
Imetolewa na:
Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile (Mb.)
NAIBU WAZIRI
03/01/2018

0 Comments