NA TIGANYA VINCENT-RS TABORA
SERIKALI ya Wilaya ya Urambo imepiga marufuku ukusanyaji wa mapato yote kwa kutumia stakabadhi ya kuandika (ngalawa) kwa kuwa ndio zinasababisha washindwe kufikia lengo kwa kutoa mwanya wa wizi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa wakati Mkutano Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wa kujadili mpango wa bajeti wa mwaka 2018/19
Alisema Mtendaji yoyote atakayekutwa anakusanya mapato ya Serikali kinyume na maagizo ya viongozi wa juu ya kutumia mashine ya kielektroniki (EFD) atachukuliwa hatua kali.
Kwingwa alisema matumizi ya stakabadhi ya kuandika badala ya mashine ndio usababisha mapato mengi ya Serikali kupotea na Halmashauri kushindwa kufikia lengo ililojiwekea.
Alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kuhakikisha katika kila eneo ambalo ni chanzo cha mapato kwa Halmashauri hiyo liwe na mashine ya EFD kwa ajili ukusanyaji wa mapato.
Kwingwa aliwataka watendaji wanahusika na ukusanyaji wa mapato kuhamia katika maeneo yanayotumika kwa kama vyanzo vya mapato ili kusimamia ukusanyaji na sio kushinda maofisini wakiwa kwenye Kompyuta.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alilishauri Baraza la Madiwani na Watenadji wa Halmashauri ya Urambo kuongeza idadi ya minada walau kila Kata ili kuwepo mapato mapya ambayo yatasaidia katika uboreshaji wa huduma za jamii.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Adamu Malunkwi alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha anampangia kila Mkuu wa Idara kuwa na chanzo cha kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kikifanya vibaya aweze kuwajibika.
Malunkwi alisema Mkuu wa Idara atakayefanya vibaya katika eneo lake itabidi aeleze kwa nini ameshindwa kufikia lengo.
Alisema utaratibu huo ndio utawasaidia kuvuka lengo ambalo waliagizwa na Waziri Mkuu la kukusanya zaidi ya asilimia 80 ambapo hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Januari tayari walikuwa wameshakusanya asilimia 50.
Malunkwi alisema kuwa licha ushuru wa mazao kushuka kutoka asilimia tano hadi tatu na mauzo ya tumbaku msimu uliopita yalikuwa mabaya kwa baadhi ya wakulima hadi hivi kutouza tumbaku yao wanatumaini kufikia lengo.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Halmashauri aliwaomba Madiwani kusaidia kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ili lengo liweze kufikiwa.
Waziri Mkuu akiwa ziarani Tabora alizitaka Halmashauri ambazo zimeshindwa kukusanya mapato ya ndani na kufikia asilimia 80 zijieleze na kusema kuwa zitakazoendelea kufanya vibaya atalazimika kuzivunja.

0 Comments