Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inajitahidi kujenga na
kutanua vituo vya Afya ikiwa na lengo la kupunguza msongamano kwenye hospitali
za Wilaya.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa
kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa
kituo cha Afya Ihongole kilichopo mjini Mafinga.
Makamu wa Rais ambaye yupo kwenye ziara ya
kuhamasisha shughuli za kimaendeleo mkoani Iringa ambapo leo alitembele wilaya
ya Mufindi na kuweka mawe ya msingi katika miradi miwili ikiwa mmoja ni wa
kujenga maabara ya kisasa na madarasa na kidato cha tano na cha sita katika
Sekondari ya Mgololo na upanuzi wa kituo cha Afya cha Ihongole kilichopo
Mafinga.
Akiwahutubia wananchi waliojitokeza
kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la
Upanuzi wa kituo cha Afya Ihongole , Makamu wa Rais alisema katika kila kituo
cha afya kinachopanuliwa ama kujengwa Serikali imezingatia huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo
vya akinamama na watoto, kuborsha huduma za upasuaji .
Serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa
ajili ya upanuzi wa kituo hicho na kutumia mafundi wa kawaida kujenga ilikuweza
kusaidia kutoa ajira kwa vijana zaidi wa eneo husika.
Makamu wa Rais amezitaka halmashauri
zisimamie utoaji na matumizi ya fedha wanazotoa kwa Vijana asilimia 5 na
Wanawake asilimia 5 ili kuleta tija kwenye shughuli za maendeleo.
Makamu wa Rais alisema “tunapozungumzia uchumi
wa viwanda lazima tuwaandae Vijana tangia wadogo, tuhakikishe
wanafundishwa yale yanayohitajika”.
Makamu wa Rais aliwaambia wakazi wa
Mafinga, watakapokuja tena kwenye kampeni watawataka wananchi waseme Serikali
yao imewafanyia nini.
Mapema leo Makamu wa Rais aliweka jiwe la
msingi la ujenzi wa maabara na madarasa
ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Mgololo, ujenzi
ambao utagharimu shilingi milioni 450 za kitanzania chini ya ufadhili wa
kiwanda cha Mufindi Paper Mills.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa Mafinga waliojitokeza kwenye uwekaji
wa jiwe la msingi la upanuzi wa kituo cha Afya cha Ihongole. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la upanuzi wa ujenzi wa kituo cha afya Ihongole Mafinga, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza.
(picha na ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisoma maneno yalioandikwa kwenye jiwe la msingi la ujenzi wa maabara na madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Mgololo, Mufindi mkoani Iringa mara baada ya kulifungua ,pembeni yake ni Mwenyekiti wa Makampuni ya Rai wanaomiliki kiwanda cha Mufindi Paper Mills Bw. Jaswant S. Rai na kulia ni Mkuu wa mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)



0 Comments