Waogeleaji wakichuana katika staili mbalimbali mbali.
Katibu Mkuu wa Dar Swim Club (DSC), Inviolata Itatiro (Kulia) na Meneja Mkuu wa Taliss Jone Gouws.
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Mashindano ya kuogelea ya wazi ya Taliss yataanza Ijumaa kwa kushirikisha waogeleaji kutoka klabu 11 za Tanzania Bara na Zanzibar.
Mashindano hayo yamepangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Upanga, mbali ya klabu kutoka Zanzibar, pia yatashirikisha klabu kutoka mikoa ya Morogoro, Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam.
Kocha maarufu wa mchezo wa kuogelea nchini, Alex Mwaipasi alizitaja klabu hizo kuwa ni Dar Swim Club (DSC), Bluefins, Mwanza Swim Club, Geita Gold International school, IST Tanganyika, ISM-Moshi na Arusha Swim Club.
Klabu nyingine kwa mujibu wa Mwaipasi ni Wahoo ya Zanzibar, Champion Rise, Morogoro Swim Club na wenyeji, Taliss.
Waogeleaji kutoka klabu watashindana katika staili mbalimbaliambazo ni freestyle, Breaststroke, Butterfly, Backstroke na Individual Medlay (IM) kwa umbali wa mita 50, 100 , 200 na 400.
Mbali ya ushindani wa muogeleaji mmoja mmoja, pia kutakuwa na mashindano ya kuogelea kwa kupokezani (relay) mchanganyiko (wanawake na wanaume ) na relay za wanaume na wanawake pekee.
Alisema kuwa siku ya kwanza ya mashindano, waogeleaji watachuana kwa mita 200 na 400 katika staili tofauti kuanzia saa 9.30 alasiri na na siku ya pili watashindani kuanzia mita 50, 100 na nyinginezo.
“Maandalizi yamekamilika na washindi watazawadiwa medali, vikombe na vyeti mbalimbali, madhumuni yetu ni kuendeleza mchezo wa kuogelea kwa upande wa vilabu na Taifa kwa ujumla pamoja na matatizo yaliyopo,” alisema Mwaipasi.
Alisema pia kutakuwa na zawadi za vikombe kwa timu tatu za kwanza kwa upande wa wanawake na wanaume na zaidi za mshindi wa jumla.



0 Comments