Baadhi ya watoto waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza kifaa cha
usikivu jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakicheza karata leo.
Watoto hao wanaendelea vizuri na matibabu baada ya upasuaji huo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua na Masikio na Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Pua na Masikio wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt
Edwin Liyombo akipandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto Raiyyan Mshana
mwenye tatizo la usikivu baada ya kumfanyia upasuaji leo. Kulia ni
Profesa Hassan Wahba kutoka Chuo Kikuu cha Tiba nchini Misri.
Picha ikionyesha jinsi Dkt. Edwin Liyombo akipandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto Raiyyan Mshana mwenye tatizo la usikivu.
Dkt Liyombo akizungumza na
waandishi wa habari leo kuhusu watoto waliopandikizwa vifaa vya usikivu
baada ya kufanyiwa upasuaji wa masikio.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili
………………
Watoto
sita wenye tatizo la kutosikia wamefanyiwa upasuaji na kupandikizwa
vifaa vya usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Upasuaji
huo umeanza Januari 29, mwaka huu na umehusisha wataalam wa Muhimbili
kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Cairo, Misri.
Daktari
Bingwa wa Masikio, Pua na Koo Dkt. Edwin Liyombo amesema hii ni ni mara
ya pili kwa upasuaji huo kufanyika Muhimbili, upasuaji wa kwanza
ulifanyika Juni mwaka jana ambapo watoto watano waliwekewa vifaa hivyo.
Akisisitiza
amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutekeleza azma ya
serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi
ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa
nchini ama kutokana na kutokuwepo kwa wataalam au ukosefu wa vifaa vya
kutolea huduma husika.
“Takwimu
za MNH zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji
kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo ,
hivyo huduma hii itasaidia watoto wengi hapa nchini lakini pia inazidi
kuwajengea uwezo wataalam wetu wa ndani’’ amesema Dkt. Liyombo.
Kwa
mujibu wa Dkt. Liyombo, kupeleka mtoto mmoja nje ya nchi kwa ajili ya
kupandikizwa kifaa cha usikivu ni kati ya Shilingi milioni 85 hadi
Shilingi milioni 100 wakati gharama ya upasuaji kwa mtoto mmoja katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili ni shilingi milioni 33.
Akielezea
ukubwa wa tatizo la kutosikia amesema kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa,
watoto watano wanazaliwa na tatizo la kutosikia hivyo kutokana na
hali hiyo wazazi wanapaswa kujenga tabia ya kuwapeleka watoto wao
hospitalini ili kubaini tatizo mapema.
Katika
Hospitali za Umma, Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa huduma ya
upandikizaji wa vifaa vya usikivu na ya pili kutoa huduma hiyo katika
nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na Kenya.




0 Comments