Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto)
akipatiwa taarifa ya hali ya hewa kwa usafiri wa anga na Meneja wa Utabiri wa
Hali ya Hewa Bwana Samwel Mbuya wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati
alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akipatiwa maelezo na
msomaji wa taarifa ya hali ya hewa kwenye vituo mbalimbali vya televisheni Bi.
Hellen Msemo kuhusu namna wanavyotoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa wakati
alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es
Salaam
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akizungumza na
Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati alipotembelea
makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi
hiyo Dkt. Buruhani Nyenzi na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo
Dkt. Hamza Kabelwa
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha za
usafiri wa anga na majini ambazo usafiri wake unategemea utabiri wa hali ya
hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha ya
ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendokasi ambapo ujenzi wa miundombinu ya
barabara, reli unategemea utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao
makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Nditiye (hayupo pichani) akiangalia picha ya
rada ya hali ya hewa iliyopo kwenye vituo vya
utabiri wa hali ya hewa wakati alipotembelea makao makuu ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye ameilekeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kujitangaza
umuhimu wake katika nyanja ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na taifa kwa
ujumla. Mhandisi Nditiye ameyasema hayo alipotembelea makao makuu ya TMA na
kuzungumza na bodi ya Mamlaka hiyo, menejimenti na wafanyakazi kwa lengo la
kutambua majukumu yao na kufuatilia utekelezaji wake ili kufikia malengo ya
Serikali ya kuwatumikia wananchi.
Akizungumza na Bodi,
menejimenti na wafanyakazi, Mhandisi Nditiye amewaeleza kuwa TMA ni chombo
muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa letu na wananchi kwa
ujumla kwa kuwa sekta ya usafiri wa anga, majini, ujenzi wa majengo mbalimbali,
miundombinu ya barabara na reli, afya, kilimo na mazingira vyote vinategemea
taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye Mamlaka hii.
“Mtambue kuwa hakuna ndege
inayoweza kutua wala kuruka bila kupata taarifa kutoka kwenu, vile vile
mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ya SGR nae anategemea taarifa zenu kwa
kiasi kikubwa, hivyo mtambue ninyi ni muhimu na mjitangaze,” amesema Mhandisi
Nditiye.
Amesisitiza kuwa ni
vema mjitangaze ili wananchi na wadau mbalimbali wafahamu majukumu na umuhimu
wa taasisi yenu kwa kuwa uchumi wa taifa hili unategemea taarifa zenu ambapo
wananchi wengi wamezoea kusikia na kuwaona mkitoa taarifa za tahadhari za hali
ya hewa zinazohusiana na majanga na matukio mengine yanayohusiana na utabiri
wenu angali ninyi mna taarifa muhimu zaidi na tofauti na mtazamo wa wananchi
walio wengi.
Amefafanua kuwa
wananchi wanaziamini taarifa zenu za hali ya hewa kwa kuwa kwa kiasi kikubwa
yale mnayotabiri na kuwaeleza ndiyo yanayotokea iwe ni mvua kubwa, upepo mkali
au joto kali kama ilivyo sasa.
“Nimetembea na kukagua mitambo, vifaa vya kisasa
na namna wanavyofanya kazi na nimebaini kuwa taarifa zinazotolewa hapa
zimekusanywa kutoka vituo mbali mbali vya hali ya hewa nchini ambapo hapa makao
makuu wataalamu wanazichakata, kusambaza kwa wahusika na kuhifadhiwa, na
zinaonesha kuwa ni taarifa za uhakika kwa kiwango cha asilimia 87.5 ambapo
imeongezeka kutoka asilimia 82.1 kwa miaka mitatu iliyopita,” amesema Mhandisi
Nditiye.
Mwenyekiti wa Bodi ya
TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye amesema
kuwa Mamlaka hii ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu na wananchi
kwa ujumla kwa kuwa utoaji wa taarifa na huduma za hali ya hewa nchini
zimewezesha uokoaji wa maisha ya watu na mali zao; kuepuka au kupunguza athari
na hasara zinazosababishwa na matukio ya hali ya hewa; kuongeza tija na
mafanikio katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi; kuwa na
miundombinu imara kama vile barabara, madaraja; kuongeza ufanisi katika sekta
za usafiri na mawasiliano; kuchangia katika sekta za ujenzi na uendeshaji wa
viwanda nchini na kukuza pato la taifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TMA Dkt. Hamza Kabelwa amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa wahitaji wa
taarifa za hali ya hewa kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali ambao wanahitaji
kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii wamekuwa wengi na
teknolojia ya utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa taarifa zake umebadilika
ambapo inatulazimu kuhuisha Sheria Na. 6 ya Hali ya Hewa ya Mwaka 1978 na
kukamilisha Sera ya Taifa ya Hali ya Hewa ili ziweze kwenda na wakati pamoja na
kuboresha chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kwa kuwa ndio chuo pekee nchini
kinachotoa elimu ya awali na ya kati ya hali ya hewa.
Ameongeza kuwa TMA
imepatiwa cheti cha ubora wa utoaji huduma na Shirika la Viwango la Kimataifa
(ISO) kwa kutoa huduma kwa sekta ya anga nchini. Pia, inashirikiana na Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa jangwa la
Afrika (SADC), Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Hali ya
Hewa Duniani (WMO) kwa kubadilishana taarifa za hali ya hewa, mabadiliko ya
hali ya hewa yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa, na kuendeleza na kutunza
mtandao wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa ili kukidhi makubaliano ya
kimataifa ya kubadilishana taarifa hizo.
Dkt. Nyenzi
amemshukuru Mhandisi Nditiye na kumueleza kuwa TMA inafarijika kusikia kuwa
anafahamu kwa undani umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa nchini, hivyo ni imani
yake kuwa ataisamimia vema ili ifikie malengo.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 Comments