Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri.
NA TIGANYA VINCENT RS-TABORA
UONGOZI wa Mkoa wa Tabora umewaagiza viongozi wa Wilaya za Igunga na Nzega kuwahimiza wakazi maeneo hayo kulima kwa wingi zao la pamba na mazao mengine yanayohimili ukame ili kuepuka hasara wanayopata kwa kung’ang’ania kulima mahindi ambayo kwa kiasi kikubwa havuni.
Kauli hiyo imetolewa jana katika maeneo tofauti wilayani Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa kampeni ya uelimishaji wakulima wa zao la pamba juu ya upigaji wa dawa sahihi za kuua wadudu waharibifu katika zao hilo.
Alisema wakulima wa Igunga na Nzega kila mwaka wanang’ang’ania kulima mahindi lakini zao hilo limeishia katika kukauka bila kukomaa pindi mvua inaposimama na hivyo kujikuta wamepoteza muda na nguvu nyingi bila mafanikio.
Mwanri alisema kama wanahitaji mahindi ya kuchoma sio lazima walime mashamba makubwa wanapaswa kulima walau hata nusu ekari na eneo liliobaki walime pamba na mazao mengine kama vile mtama , uwele , viazi na mihogo ambayo ni yanayohimili ukame na ni msaada kwa chakula.
Alisema kama wanahitaji mahindi ya chakula wanatakiwa kulima pamba kwa wingi ili pesa watakazopata ziwasaidie katika ununuzi wa zao hilo kulima wanavyopteza nguvu nyingi bila mafanikio .
“Tumeona katika mashamba mbalimbali tuliyopita mahindi yamekauka baada ya mvua kusimama kwa wiki nne hivi karibuni…hakuna matumaini tena ya wakulima walio wengi wa Nzega na Igunga kuvuna mahindi…mahindi waachieni Urambo, Kaliua, Sikonge na Uyui…mkipata pesa za pamba mtanunua kutoka kwao”alisema Mwanri.
Alisema kitendo cha wao kuendelea kulima mahindi kila mwaka bila mafanikio hakiwasaidia kuwaletea maendeleo bali kitazidi kuwarudisha nyuma kila mwaka.
“Hapa limeni mtama,uwele, viazi , mihogo na mpunga katika mabonde na maboga lakini mahindi naomba msahau kwa kuwa kila mwaka nawaona mnakazania kulima mahindi lakini hampati kitu” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa kuanzia sasa kila zao mkoani humo litalimwa kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora na sio kinyume cha hapo.
Alisema lengo ni kutaka wakulima kuzalisha mazao yaliyo bora na mengi ili yaweze kuwainua kiuchumi na kuwaletea maendeleo.
Mwanri aliwaagiza Maofisa Ugani kuanza mara moja kutoa elimu kwa wakulima juu ya ulimaji wa mazao mbalimbali kwa kuzingatia kanuni bora.
Alisema baada ya elimu hiyo mkulima atakayekiuka atachukuliwa hatua za kukwamisha maendeleo yake na jamii.

0 Comments