Random Posts

Serikali ya Israel imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

Waziri wa ulinzi wa Israel Mhe. Avigdor Liberman  akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuona ushirikiano ulipo wa matibabu ya moyo kwa watoto, kusomesha madaktari na wauguzi kati  ya JKCI na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel. Kulia ni waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee  na watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

Na Mwandishi wetu

Serikali ya Israel imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuongeza  utoaji wa huduma bora za matibabu  kwa watoto wenye matatizo ya moyo hapa nchini.
Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri wa ulinzi wa Israel Mhe. Avigdor Liberman  alipotembelea JKCI   kwa ajili ya kuona ushirikiano ulipo kati ya Taasisi hiyo na   Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) ya nchini Israel.
Mhe. Avigdor Liberman  alipogeza mafanikio ambayo JKCI imeyapata katika utoaji wa huduma ya matibabu ya moyo na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi ili wananchi wenye matatizo ya moyo waweze kupata huduma bora.
Kwa upande wake  waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee  na watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliishukuru Serikali ya Israel kwa mchango  mkubwa wanaoutoa wa kuimarisha huduma ya matibabu ya kibingwa katika magonjwa ya moyo.
 Mhe. Ummy alisema miaka ya nyuma  kabla ya kuanza kwa ushirikiano huo kati ya  wagonjwa mia moja waliokuwa wanahitajo kufanyiwa upasuaji wa moyo wagonjwa themanini walipelekwa  nje ya nchi, lakini hivi sasa kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu imepungua na badala yake wanatibiwa hapa nchini.
“Licha ya kwamba tunawapeleka  madaktari bingwa nchini  Israeli lakini pia madaktari bigwa kutoka Israeli wanakuja Tanzania kuongeza ujuzi kwa madaktari wetu katika kufanya upasuaji  na uchunguzi.”
“Kwa mfano miaka mitano iliyopita asilimia thelathini ya upasuaji uliokuwa unafanywa nchini ulikua unafanywa na madaktari wetu lakini kutokana na ushirikiano kutoka Serikali ya Israeli hivi sasa madaktari wetu wanafanya upasuaji kwa asilimia sitini na tano na madaktari wa nje ni asilimia thelathini na tano ambapo  ni ongezeko mara mbili.
Naye Mkurungenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed  Janabi alisema kadri madaktari  wanapotapa mafunzo zaidi ndivyo wanavyoofanya upasuaji mara nyingi zaidi.
Prof. Janabi alisema   katika kipindi cha miaka mitango ijayo  watakuwa wamepandisha asilimia kubwa ya upasuaji wa moyo ila wanajua hawawezi kufikia asilimia mia moja kwasababu ujuzi wa wataalamu wa nje unaongezeka kila siku lakini watafikia angalau asilimia themanini mpaka themanini na tano ya upasuaji.
Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza ushirikiano na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto kwa kufanya  kambi maalum za matibabu ya moyo kwa watoto ambapo watoto wanaokutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya hali ya juu wanatibiwa nchini Israel bila malipo.

Post a Comment

0 Comments