Baadhi ya mifugo wakiwa katika eneo la kunywa maji kablaya
kuuzwa katika Soko la Kimkakati la Longido, Wilayani Longido amablo
limejengwa kwa ufadhili wa Programu ya Miundo mbinu ya Masoko,
Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
Sehemu
ya kunyweshea mifugo iliyojengwa katika Soko la Kimkakati la Longido,
Wilayani Longido kwa ufadhili wa Programu ya Miundo mbinu ya Masoko,
Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
Serikali kupitia, Programu ya
Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARF), imetekeleza maombi 5 ambayo yanawasaidia wafugaji hao
kuongeza thamani ya mifugo yao kupitia Soko la Kimkakati la mifugo
Longido lililojengwa na Program hiyo.
Mwishoni mwa mwaka 2017, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira ,Kazi, Vijana na Watu
wenye Ulemavu ) Mhe.Jenista Mhagama, alikuwa na ziara ya kukagua ujenzi
wa soko hilo wilayani humo, ambapo baada ya ukaguzi alikutana na
wafanyabiashara ya mifugo, ambao waliwasilisha maombi 5, ambayo
yangeweza kuongeza Thamani Biashara za Mifugo na kutatua kero zote za
wafanyabiashara wa mifugo wilayani humo.
“Serikali ya awamu ya tano
imeamua kuwasikiliza watu wanyonge na ambao wanajituma kuchapa kazi,
lakini pia lengo la Program ya MIVARF ni kuongeza kipato kwa wananchi
hasa waishio vijijini, kwa mantiki hiyo nilimuelekeza Mratibu wa Program
Kutekeleza maombi yao haraka sana ili wafugaji hawa wapate tija ya
ufugaji kupitia soko hili” alisema Mhagama
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa
Mifugo wilayani Longido, Saruni Laizer amesema maombi waliyowasilisha
serikalini ili waweze kupata tija ya mifugo kupitia soko la Kimkakati la
Mifugo Longido yamefanyiwa kazi na Program ya MIVARF ndani ya miezi
mitatu tangu wayasilishe, ikiwa ni; Mizani ya kupima mifugo, Maji ya
kunyweshea mifugo, machinjio, Josho, pamoja na umeme.
“Tulihitaji maji hapa ili
mifugo isije ikafa wakati inasubiri kuuzwa kwa kukosa maji, lakini umeme
hapa ni muhimu kwani biashara zetu zinafanyika usiku, tayari hadi
jenereta imeletwa kwa ajili ya kuhakikisha biashara haikwami kwa dharura
yoyote ile, lakini mizani itasaidia kutowauza mifugo kwa kuangalia kwa
macho bali kwa uzito wao” alisema Laizer
Mhagama alitoa maagizo hayo baada
ya kukagua Soko la kimkakati lililojengwa na Serikali kupitia Ofisi
Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Programu ya Miundo mbinu ya Masoko,
Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF).
Soko hilo litawanufaisha wananchi
wapatao 14,2000 wa wilayani Longido ambapo asilimia 95 ni wafugaji na
wanaojishughulisha na biashara za mifugo.
Soko hilo la kimkakati ambalo
halijafunguliwa rasmi , tayari halmashauri ya wilaya hiyo imeweza
kukusanya mapato ya kiasi cha shilingi milioni 106 kwa mwaka 2016/2017
ambapo kwa makusanyo hayo yamewezesha halmashauri hiyo kuvunja rekodi ya
miaka kumi iliyopita kwa kukusanya shilingi bilioni 1.3 kwa mara ya
kwanza kwani awali mapato yake yalikuwa chini ya bilioni moja.
MIVARF; ni Programu ya Miundo
Mbinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini iliyobuniwa na serikali
ya Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya
Kilimo yaani (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Programu
hii inatekelezwa katika mikoa 29 ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani
tangu mwaka 2011.


0 Comments