Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akipokelwa na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudensi Milanzi mjini Dodoma jana
ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 25 wa Baraza la wafanyakazi
wa Wizara hiyo.
.............................. .............................. .................
Tanzania
imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi
kufikia 1,327,143 mwaka 2017 hali iliyopelekea kuongezeka kwa mapato
ya Serikali.
Akizungumza
wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili
na Utalii uliofanyika mjini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Hamisi
Kigwangalla amesema Wizara yake itaendelea kuvutia watalii wengi zaidi
ili kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa.
“Mapato
yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni
2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Kimarekani Bilioni 2.2 mwaka 2017” alisema
Dk. Kigwangalla.
Akifafanua
Dkt. Kigwangala amesema lengo la Serikali ni kuona mafanikio haya
yanazidi kuimarika, hivyo kila mtumishi katika Wizara hiyo lazima
atimize wajibu wake ipasavyo katika kutimiza lengo la Wizara hiyo
ambalo ni kuhifadhi na kusimamia maliasili, malikale na kuendeleza
utalii.
Aliongeza
kuwa ili kufanikisha majukumu ya Wizara hiyo ipasavyo ni muhimu kuwa na
bajeti ambayo itawezesha kushughulikia changamoto za migogoro ya mipaka
katika maeneo ya hifadhi, kufanya mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni
mbalimbali, upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi, kutoa elimu
ya maadili na kusimamia watumishi.
Alisema
Wizara yake itaendelea na mapambano dhidi ya ujangili, biashara haramu
ya nyara, magogo na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria
kwa watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma
kwa kushiriki katika vitendo hivyo.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudensi Milanzi
amesema kuwa Wizara hiyo itazingatia ushauri utakaotolewa na Baraza la
Wafanyakazi wa Wizara hiyo ili kuongeza tija katika kutatua changamoto
zinazojitokeza.
“Wizara
itaendelea kupambana dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara na
magogo na kuwachukulia hatua kali watumishi wote watakaogundulika
kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo “
Alisisitiza Meja Jenerali Milanzi.
Wizara
kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliendelea na utaratibu wa kuendeleza
watumishi katika mafunzo ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:-Jumla ya
watumishi wanne (4) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje na ndani.
Aidha, mtumishi mmoja(1) yupo nje ya nchi.
Watumishi wengine kumi na moja (11) walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Mafunzo haya yalihusu watumishi wa kada mbalimbali.
Jumla
ya watumishi saba (7) wamehudhuria mafunzo ya ujasiliamali unaohusiana
na maandalizi ya kustaafu. Aidha, Wizara bado inaendelea na utaratibu wa
kuwaandaa watumishi wote wanaokaribia kustaafu kuhakikisha wanapata
mafunzo hayo.
Akifunga
mkutano huo wa siku moja Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Japhet
Hasunga aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii,
juhudi na maarifa ili kufikia lengo lililokusudiwa la uhifadhi wa
maliasili, malikale na kuendeleza Utalii.
Waziri wa Mali Asili
na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akihutubia Wafanyakazi wa Wizara
hiyo wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo
uliofanyika mjini Dodoma jana.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudensi Milanzi akizungumza na Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wa baraza wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. HamisI KigwangalLa (katikati) akiimba
wimbo wa mshikamano pamoja na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Maj. Gen.
Gaudensi Milanzi pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la
Wafanyakazi.
Baadhi
ya ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Wakiimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi wakati wa mkutano huo
uliofanyika mjini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto)
akisalimiana na Katibu Mteule wa Tughe Tawi la Wizara ya Maliasili na
Utalii, William Mwita muda alipowasili kufunga mkutano huo wa baraza.
Katikati anayemtambulisha kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na
Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
Naibu
Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo
na Katibu Mkuu Wizara wizara hiyo, Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi
muda mfupi kabla ya kufunga mkutano huo wa baraza la wafanyakazi wa
wizara hiyo.
Naibu
Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza
na watumishi wa wizara hiyo wakatika akifunga mkutano huo wa baraza la
wafanyakazi wa wizara hiyo.
Baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara hiyo walioshiriki baraza hilo.
Baadhi ya watumishi wa Wizara na wajumbe wa baraza hilo.






0 Comments