Meneja Mwandamizi wa kiwanda cha
kuzalisha mita za LUKU cha Inhemeter Tanzania Limited, Will Tang (kulia)
akielezea majukumu ya kiwanda hicho kwa Kamishna wa Nishati,
Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) katika ziara yake aliyoifanya katika kiwanda hicho
kilichopo jijini Dar es Salaam tarehe 03
Aprili, 2018.
Kamishna wa Nishati,
Mhandisi Innocent Luoga (katikati) akitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda hicho. Kushoto ni Mshauri
Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt. Adelhelm Meru na kulia ni Meneja Mwandamizi
wa kiwanda hicho,Will Tang.
Mafundi wakiendelea na kazi ya
kutengeneza mita katika kiwanda hicho.
Mtambo maaalum wa kupima ubora wa
mita katika kiwanda hicho.
Kutoka kushoto mbele Meneja
Mwandamizi wa kiwanda cha kuzalisha mita za LUKU cha Inhemeter Tanzania
Limited, Will Tang Kamishna wa Nishati, Mhandisi
Innocent Luoga, Mshauri Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt.
Adelhelm Meru na Msimamizi wa Utawala wa kiwanda hicho, Khilna Chohan wakiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Baadhi ya mita za LUKU zinazotengenezwa na kiwanda hicho.
Na
Greyson Mwase, Dar es Salaam
Tarehe 03 Aprili, 2018 Kamishna wa Nishati,
Mhandisi Innocent Luoga alifanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha mita za LUKU
cha Inhemeter Tanzania Limited kilichopo jijini Dar es Salaam.
Lengo la zira hiyo lilikuwa ni kuangalia utendaji
kazi wa kiwanda hicho pamoja na kutatua changamoto zilizopo katika kiwanda
hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo Mshauri Mkuu wa
Kiwanda hicho, Mhadisi Dkt. Adelhelm Meru alisema kiwanda hicho
kilichoanzishwa Februari mwaka huu kina uwezo wa kuzalisha mita 500,000 kwa
mwaka na kusisitiza kina uwezo kwa kuzalisha hadi mita milioni moja kulingana
na mahitaji ya soko.
Dkt Meru aliendelea kusema kuwa, kiwanda kimeanza
kuzalisha mita kidogo na kuiomba serikali kupitia Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa
miundombinu ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa
oda za mita nyingi ili waanze kuzalisha mita nyingi za kutosha kulingana na
soko.
"Mita tunazotengeneza zina ubora wa hali ya
juu zenye kuendana na mazingira ya aina yoyote, tunaunga mkono juhudi za
Serikali kuelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa kusambaza vifaa kwa ajili ya
wakandarasi wanaojenga miundombinu ya umeme nchini,"alisema Dkt. Meru.
Wakati huohuo Meneja Mwandamizi wa Kampuni hiyo,
Will Tang aliomba Serikali kutoa kipaumbele kwa matumizi ya vifaa vya umeme
vinavyotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi.
Naye Mhandisi Luoga aliuhakikishia uongozi wa
kiwanda hicho kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaunga mkono juhudi za
kiwanda hicho na kusisitiza kuwa ipo tayari kutumia bidhaa zake katika miradi
ya umeme vijijini.
"Mara baada ya kuthibitisha ubora wa bidhaa
zenu, mnatakiwa kujiandaa kupokea oda kubwa kutoka TANESCO na REA kwa
mwaka," aliongeza Kamishna Luoga.
Alisema katika kuhamasisha Sera yake ya Uchumi wa
Viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano inatoa kipaumbele cha matumizi ya bidhaa za
ndani hususan katika miradi ya umeme nchini kwa kuwa viwanda vya ndani
vitaongeza mapato, ajira na hata kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa bei
nafuu nchini.
Akielezea hatua kadhaa zilizochukuliwa na Serikali
kupitia Wizara ya Nishati kwenye uhamasishaji wa uwekezaji wa viwanda vya
ndani, Mhandisi Luoga alieleza kuwa, Serikali imepiga marufuku uingizaji wa
nguzo za umeme kutoka nje ya nchi pamoja na bidhaa nyingine zinazopatikana hapa
nchini.
"Tunataka ifike mahali mita za LUKU,
transfoma, nyaya na vifaa vingine vyote vya umeme vitoke ndani ya nchi tu na
kukuza uchumi wa viwanda," alisisitiza Mhandisi Luoga.
Hata hivyo Mhandisi Luoga alielekeza kampuni hiyo
kukaa pamoja na Wizara, TANESCO na REA na kupanga namna ya kushirikiana katika
utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme nchini.






0 Comments