Ndugu Wananchi
Siku ya Afya duniani
huadhimishwa tarehe 7 Aprili ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni HUDUMA
BORA ZA AFYA KWA WOTE.
Kauli mbiu inatutaka
kuhakikisha kuwa hukuna mtu anayekosa huduma za afya popote alipo. Napenda
kuchukua fursa hii kuwafahamisha wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mhe Rais Dr. John Pombe Magufuli inaendelea kuchukua hatua
mahususi za kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa kila mtanzania
mahali popote alipo bila kikwazo.
Hatua tulizochukua ni pamoja na
kuongeza rasilimali fedha kwa kugharamia huduma za afya, kuimarisha huduma za
chanjo kwa watoto, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ikiwemo huduma za
uzazi za dharura, kupanua huduma za matibabu ya kibingwa sambamba na kuimarisha
mifumo ya kutoa huduma za afya.
Ndugu wananchi
Tangu tumepata Uhuru,
Serikali imehakikisha inawapatia wananchi wake huduma bora za Afya bila kikwazo
cha aina yoyote. Katika kuhakikisha dhana hii ya Upatikanaji wa huduma za afya
kwa wote na kwa uhakika (Universal Health Coverage – UHC), Serikali imekuwa na
mipango na mikakati mbalimbali ya kutekeleza azma hiyo.
Utekelezaji wa Mikakati
hiyo unawiana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba Matokeo ya Malengo
Endelevu ya Dunia (SDGs) na mipango ya nchi katika kuelekea uchumi wa Viwanda
na middle income
Country yanafikiwa.
Ndugu Wananchi
Serikali imekuwa
ikitoa kipaumbele kwa sekta ya Afya kwa kutenga fedha kwa ajili ya Kugharamia
utoaji wa huduma za Afya Nchini.
Kiwango cha Fedha kinachotengwa
katika Sekta ya Afya kimeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo
katika mwaka wa fedha 2016/17 Sekta ya afya ilitengewa kiasi cha shilingi
trilioni 1.9 na mwaka 2017/18 ilifikia shilingi trilioni 2.2.
Mwenendo huu unaonyesha
kumekuwepo na juhudi kubwa ya Serikali katika kuipa Sekta ya afya kipaumbele
ili iweze kutekeleza mipango ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wote.
Ndugu Wananchi
Serikali imeendelea
kuhakikisha hali ya upatikanaji wa dawa inaboreshwa katika vituo vya kutolea
huduma za afya nchini ili kuondoa kero kwa wananchi ya kukosa huduma ya dawa
wanapokwenda kutibiwa katika vituo vya umma vya kutolea huduma za Afya.
Katika mwaka 2017/18, Serikali
imetenga Kiasi cha Shilingi bilioni 269 kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa,
vifaa, vifaa tiba, na vitendanishi ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi bilioni
31 kilichotengwa mwaka 2015/2016. Hali hii imewezesha upatikanaji wa dawa
muhimu 135 katika Bohari ya Dawa (MSD) kwa kiwango cha wastani wa asilimia 81
katika kipindi cha Februari 2018. Aidha hali ya upatikanaji wa dawa katika
vituo vya kutolea huduma za afya ilifikia kuwa asilimia 89.6 katika kipindi
hicho.
Ndugu Wananchi
Wizara imeendelea
kutoa huduma za Chanjo kulingana na Sera na Miongozo. Aidha, Wizara kupitia
Mpango wa Taifa wa Chanjo, imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha kwa ajili
ya huduma za chanjo kwa watoto na makundi mengine kwa kununua na kusambaza
chanjo katika Mikoa na Halmashauri zote nchini.
Mwezi Desemba, 2017 nchi yetu
ilipongezwa kwa kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo nchi yetu
imekua miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo
kwa mwaka 2016, ambapo tuliweza kuvuka lengo kwa kufikia kiwango cha chanjo cha
asilimia 97 na kuwa nchi ya tatu kati ya nchi zinazofanya vizuri katika utoaji
wa chanjo baada ya nchi ya Zambia (99%) na Rwanda (98%)
Ndugu Wananchi
Katika kupunguza vifo
vya Wanawake wajawazito na watoto wachanga, Serikali imeendelea kuboresha
miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini na kusogeza huduma za Afya kwa
kujenga vituo vipya 268 na hivyo kufanya vituo vya kutolea huduma za Afya
kufikia 7,284 kwa hivi sasa, ikilinganishwa na vituo 7,014 vilivyokuwepo mwaka
2014/2015.
Vilevile, tumechukua hatua
za kuboresha vituo vya Afya (Health Centres) 220 kwa kushirikiana na
Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kuviwezesha kutoa huduma za uzazi za dharura kwa
kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji (Theatre), Wodi za Wazazi na
Watoto, Maabara ya damu na nyumba za watumishi ili kusogeza karibu na wananchi
huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.
Hadi Desemba 2015, ni Vituo vya
Afya vya Serikali (Health Centres) 117 tu (sawa na asilimia 21) kati ya
vituo vya Afya vya 473 vinavyoweza kutoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa
wajawazito.
Hakuna shaka kuwa jitihada hizi za Serikali ya
Awamu ya Tano za kupanua huduma za upasuaji wa dharura ni sehemu ya kuwezesha
Huduma bora za afya kwa wanawake wajawazito hasa wa vijijini.
Ndugu Wananchi,
Katika kuhakikisha
huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana kwa wananchi wengi, serikali
imeendelea na jitihada za kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa zitolewazo
nchini.
Maboresho hayo, licha ya kuwa yanalenga katika
kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya Matibabu nje ya nchi ili
kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali inaingia katika kupeleka wagonjwa nje
ya nchi ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibigwa kwa
wananchi hasa wa kipato cha chini.
Katika mwaka 2017/18 wanannchi
waliopewa rufaa matibabu nje ya nchi ni 103 ikilinganishwa na watu 304 mwaka
2016/17.
Mafanikio haya ni kutokana na maboresho
yaliyofanyika katika Hospitali zetu za Kifaifa, ambapo kwa hivi sasa zimeongeza
uwezo wa kutoa huduma za Kibingwa ambazo awali hazikuwa zikitolewa hapa nchini
na hivyo kulazimu wagonjwa kupatiwa rufaa nje ya nchi.
Huduma zilizoimarishwa ni pamoja
na upandikizaji wa figo na vifaa vya kuongeza usikivu (Conchlea implants)
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji kwa kutumia tundu dogo na
kufungua kifua katika Taasisi ya Jakaya Kikwete, Vilevile Serikali imeendelea
kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Taasisi ya Saratani
Ocean Road ambapo dawa zinapatikana kwa asilimia 100 na muda wa kupata huduma
ya mionzi ya Saratani imepungua kutoka muda wa miezi mitatu hadi wiki 6.
Ndugu Wananchi
Ili kufanikisha
upatikanaji wa huduma za Afya kwa kila mwananchi, Serikali kupitia Wizara ya
afya imeboresha mwongozo wa utoaji huduma katika ngazi ya Jamii. Mwongozo huu
unatoa fursa ya kuwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao watafanya kazi
chini ya usimamizi wa mkuu wa kituo cha afya yaani Zahanati, hadi sasa tuna
wahitimu 8,857.
Ndugu Wananchi
Serikali ina mpango
wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanajiunga katika mfumo wa Bima ya afya ili
wawe na uhakika wa kupata huduma za afya pindi wanapozihitaji bila ya kikwazo
cha fedha.
Lengo ya Serikali ni kuhakikisha
angalau asilimia 70 ya wananchi wote wanajiunga na kuchangia katika mfuko wa
Bima ya Afya ifikapo mwaka 2020 kutoka asilimia 32 ya sasa.
Katika kutekeleza azma hiyo,
Serikali imedhamiria kutunga Sheria itakayoanzisha Mfuko mmoja wa Bima ya Afya
ambao kila mwananchi atapaswa kujiunga na kuchangia.
Hitimisho:
Katika kuadhimisha
Siku ya Afya Duniani 2018, nitumie fursa hii kusisitiza tena kuwa ni dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi atakayekosa
huduma za bora za afya pindi anapozihitaji.
Asanteni.

0 Comments