*Asisitiza mapambano
dhidi ya viashiria vya uvunjifu wa amani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini
popote walipo wahakikishe wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwa ni
pamoja na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 31, 2018) kwenye Mkutano Mkuu wa BAKWATA
uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu wasaidizi wa Mufti wakasimamia suala hilo.
“Dini ni taasisi
muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku ndio maana Serikali inaheshimu na
kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake mkubwa katika amani ya nchi yetu.
Niwaombe viongozi wangu popote mlipo muilinde amani yetu”
Waziri Mkuu amesema
amani ni miongoni mwa neema kubwa sana kwa binadamu na ndio maana wote
wanamtambua Mwenyezi Mungu, hivyo wasiruhusu mtu au kikundi chochote kujaribu
kuchafua na kuharibu amani iliyopo nchini.
Katika
hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wahakikishe
kuwa chombo hicho kinaendelea kuwaunganisha waislamu bila ya kujali makabila
yao, rangi zao au madhehebu yao.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza wakati alipofungua Mkutano
Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwenye ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma Machi 31, 2018.
Waziri Mkuu amesema Mufti wa Tanzania Sheikh
Aboubakar bin Zubeiry ambaye ndiye kiongozi wa Waislamu nchini mara zote
amekuwa akisisitiza jambo hilo na kuwataka waislamu popote walipo watambue kuwa
hicho ni chombo chao.
“Ni muhimu sana kwa
ninyi wasaidizi wa Mufti mlio kusanyika hapa muhakikishe mnalisimamia hili
katika maeneo yenu. Katika hili napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko
pamoja Mheshimiwa Mufti kutekeleza nia hiyo njema.”
Amesema ahadi ya
Rais Dkt. Magufuli ni kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kusikiliza maoni,
ushauri na mapendekezo yeyote kutoka kwa
viongozi wa dini . ‘Milango iko wazi saa zote ‘
Ameongeza kuwa yeye
si mtaalamu sana kama walivyo Masheikh hao lakini anakumbuka maneno ya Mwenyezi
Mungu ndani ya Qur’ani sura Al Imran aya ya 103 yanayosema “ Shikamaneni na
kamba ya Mwenyezi Mungu nyote na wala msifarakane”
Mkutano huo
umehudhuriwa na Sheikh Mkuu wa Mufti wa
Tanzania Sheikh Zubeir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wajumbe wa Baraza
la Ulamaa, Masheikh na viongozi wa BAKWATA wa mikoa na wilaya zote Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI,
MACHI 31, 2018.


0 Comments